7 “ ‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale wanaotafuta uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi. 8 Nitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kutisha na cha kudharauliwa. Wote wapitao karibu watashangaa na kuudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote. 9 Nitawafanya wao kula nyama ya wana wao wa kiume na wa kike; kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzingirwa na jeshi la adui wanaotafuta uhai wao.’
10 “Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia, 11 uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi. 12 Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale wanaoishi ndani yake, asema Mwenyezi Mungu. Nitaufanya mji huu kama Tofethi. 13 Nyumba zilizo Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’ ”
14 Kisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali Mwenyezi Mungu alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la Mwenyezi Mungu na kuwaambia watu wote, 15 “Hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu, na hawakuyasikiliza maneno yangu.’ ”
<- Yeremia 18Yeremia 20 ->
Languages