1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi Mungu: 2 “Shuka uende hadi nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.” 3 Kwa hiyo nikashuka hadi nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake. 4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake; hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kwa namna alivyoona ni vyema machoni pake.
5 Kisha neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 6 “Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” asema Mwenyezi Mungu. “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, ee nyumba ya Israeli. 7 Wakati wowote nitatangaza kuwa taifa au ufalme utang’olewa, utaangushwa na kuangamizwa, 8 Lakini ikiwa taifa nililolionya litatubu na kuacha uovu wake nitaghairi, wala sitaleta maafa niliyokuwa nimekusudia kwa taifa hilo. 9 Wakati mwingine nitakapotangaza kuwa taifa au ufalme utasimikwa na kujengwa, 10 ikiwa litafanya uovu mbele zangu na halitaitii sauti yangu, nitaghairi kutenda jema nililokuwa nimekusudia.
11 “Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale wanaoishi Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tazama! Ninaandaa maafa juu yenu, nami ninapanga mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka njia zenu mbaya, kila mmoja wenu. Tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’ 12 Lakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’ ”
13 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Ulizia miongoni mwa mataifa:
Ni nani alishasikia jambo kama hili?
Jambo la kutisha sana limefanywa
na Bikira Israeli.
14 Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka
kwenye miteremko yake ya mawe wakati wowote?
Je, maji yake baridi kutoka vyanzo vilivyo mbali
yaliwahi kukoma kutiririka?
15 Lakini watu wangu wamenisahau mimi,
wanafukizia uvumba sanamu batili,
zilizowafanya wajikwae katika njia zao
na katika mapito ya zamani.
Zimewafanya wapite kwenye vichochoro
na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.
16 Nchi yao itakuwa kitu cha kutisha,
na cha kudharauliwa daima;
wote wapitao karibu nayo watashangaa
na kutikisa vichwa vyao.
17 Kama upepo unaotoka mashariki,
nitawatawanya mbele ya adui zao;
nitawapa kisogo wala sio uso,
katika siku ya maafa yao.”
18 Wakasema, “Njooni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njooni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali chochote asemacho.”