66
Kwa kiongozi wa muziki. Wimbo, Zaburi. 1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote; 2 Imbeni utukufu wa jina lake; mzitukuze sifa zake. 3 Mwambieni Mugu, “Matendo yako yanatisha kama nini! Kwa ukuu wa nguvu zako maadui zako watajisalimisha kwako. 4 Nchi yote watakuabudu wewe na watakuimbia wewe; wataliimbia jina lako.” Selah 5 Njoni na mtazame kazi za Mungu; yeye anatisha katika matendo yake awatendeayo wanadamu. 6 Aligeuza bahari kuwa nchi kavu; wao walitembea kwa mguu juu ya mto; huko tulishangilia katika yeye. 7 Yeye anatawala milele kwa nguvu zake; macho yake yanachunguza mataifa; waasi wasijivune. Selah 8 Mtukuzeni Mungu, enyi watu wa mataifa yote, sauti ya sifa zake isikike. 9 Yeye atuwekaye hai, naye hairuhusu miguu yetu iteleze. 10 Kwa maana wewe, Mungu, umetupima sisi, wewe umetupima kama inavyopimwa fedha. 11 Wewe ulituingiza sisi kwenye wavu; uliweka mzigo mzito viunoni mwetu. 12 Wewe uliwafanya watu wasafiri juu ya vichwa vyetu; tulipita motoni na majini, lakini ukatuleta mahali pa wazi palipo salama. 13 Nitaingia nyumbani mwako nikiwa na sadaka ya kuteketezwa; nitakulipa viapo vyangu 14 ambavyo midomo yangu iliahidi na kinywa changu kiliongea nilipokuwa katika dhiki. 15 Nitakutolea sadaka ya kuteketezwa ya wanyama wanene pamoja na harufu nzuri ya kondoo waume; Nitatoa ng'ombe na mbuzi. Selah 16 Njoni, msikie, ninyi nyote mnao mwabudu Mungu, nami nitatangaza yale yeye aliyoitendea roho yangu. 17 Nilimlilia kwa kinywa changu, naye alipendezwa na ulimi wangu. 18 Kama ningelikuwa na dhambi ndani ya moyo wangu, Bwana asingenisikiliza. 19 Lakini Mungu hakika amesikia; amesikia sautiya kuomba kwangu. 20 Atukuzwe Mungu, ambaye hakuyakataa maombi yangu wala kuweka uaminifu wa agano lake mbali nami.
<- Zaburi 65Zaburi 67 ->
Zaburi