141
Zaburi ya Daudi. 1 Ee Yahwe, ninakulilia wewe; uje upesi kwangu. Unisikilize nikuitapo. 2 Maombi yangu na yawe kama uvumba mbele zako; mikono yangu iliyoinuliwa na iwe kama dhabihu ya jioni. 3 Ee Yahwe, uweke mlinzi kinywani mwangu; mngojezi malangoni pa midomo yangu. 4 Usiruhusu tamaa ya moyo wangu kutamani uovu wowote wala kushiriki katika matendo ya dhambi na watu waishio maovuni. Nisile vyakula vyao vya anasa. 5 Mwenye haki na anipige; nao utakuwa ni wema kwangu. Anirudi; itakuwa kama mafuta kichwani pangu; kichwa changu na kisikatae kupokea. Lakini maombi yangu siku zote yatakuwa dhidi ya matendo yao mauvu. 6 Viongozi wao watatupwa chini toka juu mlimani; watayasikia maneno yangu kuwa ni matamu. 7 Watalazimika kusema, “Kama vile jembe moja livunjapo ardhi, hivyo mifupa yetu imesambaratishwa kinywani pa kuzimu.” 8 Hakika macho yangu yanakutazama wewe, Yahwe, Bwana; katika wewe napata kimbilio; usiiache nafsi yangu. 9 Unilinde dhidi ya mitego waliyoiweka kwa ajili yangu, na matanzi yao watendao maovu. 10 Waovu na waangukie kwenye nyavu zao wenywe pindi mimi nitorokapo.
<- Zaburi 140Zaburi 142 ->
Zaburi