Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
135
1 Msifuni Yahwe. Lisifuni jina la Yahwe. Msifuni yeye, enyi watumishi wa Yahwe, 2 ninyi msimamao katika nyumba ya Yahwe, katika nyua za nyumba ya Mungu wetu. 3 Msifuni Yahwe, kwa kuwa ni mwema; liimbieni sifa jina lake, maana ni vizuri kufanya hivyo. 4 Kwa kuwa Yahwe amemchagua Yakobo kwa ajili yake mwenyewe, Israeli kama urithi wake. 5 Najua ya kuwa Yahwe ni mkuu, na kwamba Bwana wetu yuko juu ya miungu yote. 6 Chochote Yahwe apendacho, hufanya mbinguni, duniani, katika bahari na katika vilindi vyote. 7 Hushusha mawingu kutoka mbali, akifanya mianga ya radi kuongozana na mvua na kuleta upepo toka katika ghala yake. 8 Aliua mzaliwa wa kwanza wa Misri, wote wanadamu na wanyama. 9 Alituma ishara na maajabu kati yako Misri, dhidi ya Farao na watumishi wake wote. 10 Aliwashambulia mataifa mengi na aliua wafalme wenye nguvu, 11 Sihoni mfalme wa Waamori na Ogu mfalme wa Bashani na falme zote za Kanaani. 12 Alitupatia sisi nchi yao kama urithi, urithi wa Israeli watu wake. 13 Jina lako, Yahwe, inadumu milele; Yahwe, kumbukumbu lako vizazi hata vizazi. 14 Kwa kuwa Bwana huwatetea watu wake na anahuruma juu ya watumishi wake. 15 Sanamu za mataifa ni fedha na dhahabu, kazi ya mikono ya wanadamu. 16 Sanamu hizo zina vinywa, lakini haziongei; zina macho, lakini hazioni; 17 zina masikio, lakini hazisikii, wala vinywani mwao hamna pumzi. 18 Wale wazitengenezao wanafanana nazo, vilevile kila anaye zitumainia. 19 Enyi kizazi cha Israeli, mtukuzeni Yahwe; kizazi cha Haruni, mtukuzeni Yahwe. 20 Kizazi cha Lawi, mtukuzeni Yahwe. 21 Atukuzwe Yahwe katika Sayuni, yeye aishiye Yerusalemu. Msifuni Yahwe.

<- Zaburi 134Zaburi 136 ->
  • Zaburi