1 Kisha Eliashibu, kuhani mkuu, akasimama pamoja na ndugu zake makuhani, wakajenga lango la kondoo. Walitakasa na kuweka milango yake. Waliweka wakfu hadi mnara wa Hamea na hadi mnara wa Hananeli. 2 Baada yao watu wa Yeriko walijenga, na baada yao Zakuri mwana wa Imri alijenga. 3 Wana wa Senaa wakajenga lango la samaki. Wanaweka mihimili yake na kuweka milango yake na vyuma vyake na makomeo yake. 4 Meremoth aliandaa sehemu inayofuata. Yeye ni mwana wa Uria mwana wa Hakosi. Na baada yao Meshulamu akatengeneza. Yeye ni mwana wa Berekia mwana wa Meshezabeli. Karibu nao Sadoki akatengeneza. Yeye ni mwana wa Baana. 5 Baada yao Watekoi wakatengeneza, lakini viongozi wao walikataa kufanya kazi iliyoagizwa na wakuu wao. 6 Yoyada mwana wa Pasea, na Meshulamu mwana wa Besodeya, walitengeneza lango la Kale. Wanaweka mihimili, na kuweka milango yake na vyuma vyake na makomeo yake. 7 Nao, Melatia Mgibeoni, na Yadoni Meronothi, watu wa Gibeoni na Mispa, walifanyia matengenezo juu ya sehemu ambapo mkuu wa mkoa wa ng'ambo ya Mto aliishi. 8 Na baada yake Uzieli mwana wa Harhaya, mmoja wa wafua dhahabu, akatengeneza; na baada yake Hanania, mtengenezaji wa manukato. Wakajenga tena Yerusalemu mpaka Ukuta mpana. 9 Na baada yao Refaya mwana wa Huri akajenga. Alikuwa mtawala wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu. 10 Na baada yao Yedaya mwana wa Harumafu akajenga karibu na nyumba yake. Na baada yake Hatushi mwana wa Hashabneya akajenga. 11 Malkiya mwana wa Harimu na Hashubu mwana wa Pahat Moabu, wajenga sehemu nyingine pamoja na mnara wa tanuu. 12 Baada yao Shalumu mwana wa Haloheshi, mkuu wa nusu ya wilaya ya Yerusalemu, akajenga, pamoja na binti zake. 13 Hanuni na wenyeji wa Zanoa walijenga lango la bondeni. Walijenga tena na kuweka milango yake, na vyuma vyake na makomeo yake. Walijenga dhiraa elfu hadi lango la jaa. 14 Malkiya, mwana wa Rekabu, mkuu wa wilaya ya Beth-Hakeremu, akajenga lango la jaa. Alijenga na kuweka milango yake, na vyuma vyake na makomeo yake. 15 Shalumu mwana wa Kolhoze, mkuu wa wilaya ya Mispa, akajenga lango la Chemchemi. Alijenga, na kuweka kifuniko juu yake na kuweka milango yake na vyuma vyake na makomeo yake. Alijenga upya ukuta wa Pwani wa Silowamu kwa bustani ya mfalme, hadi ngazi ya kuongoza kutoka mji wa Daudi. 16 Nehemia mwana wa Azbuki, mtawala wa nusu ya wilaya ya Beth-suri, akajenga mahali hapo, toka maburini ya Daudi, mpaka birika lililojengwa na watu, na nyumba ya watu wenye nguvu. 17 Baada yake, Walawi walijenga, pamoja na Rehumi mwana wa Bani na baada yake, Hashabia, mtawala wa nusu ya wilaya ya Keila, kwa wilaya yake. 18 Baada yake watu wa nchi zao walijenga, ikiwa ni pamoja na Binui mwana wa Henadadi, mkuu wa nusu ya wilaya ya Keila. 19 Baada yake alijenga Ezeri, mwana wa Yeshua, mtawala wa Mispa, alijenga sehemu nyingine kuelekea ghala ya silaha, kwenye kona ya ukuta. 20 Baada yake Baruki, mwana wa Zakai, akajenga kwa hiari sehemu nyingine, toka kona ya ukuta mpaka mlango wa nyumba ya Eliashibu, kuhani mkuu. 21 Baada yake Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, akajenga sehemu nyingine, toka mlango wa nyumba ya Eliashibu mpaka mwisho wa nyumba ya Eliashibu. 22 Kisha baada yake makuhani, watu wa eneo hilo karibu na Yerusalemu, walijenga. 23 Baada yao Benyamini na Hashubu walijenga kuielekea nyumba yao. Baada yao Azaria mwana wa Maaseya, mwana wa Anania, alijenga karibu na nyumba yake. 24 Baada yake Binui mwana wa Henadadi akajenga sehemu nyingine, kutoka nyumba ya Azaria hadi kona ya ukuta. 25 Palali, mwana wa Uzai, akajenga juu ya kona ya ukuta na mnara unaoenea juu kutoka nyumba ya juu ya mfalme katika uwanda wa walinzi. Baada yake Pedaya mwana wa Paroshi akajenga. 26 Sasa watumishi wa hekalu waliokaa Ofeli walijenga mpaka upande wa Hifadhi ya Maji upande wa mashariki wa mnara unaojitokeza. 27 Baada yake, Watekoi walijenga sehemu nyingine, kuelekea mnara mkubwa ulio nje, mpaka ukuta wa Ofeli. 28 Makuhani wakajenga juu ya lango la farasi, kila mmoja kuelekea nyumba yake. 29 Baada yao Sadoki, mwana wa Imeri, alijenga sehemu hiyo kuelekea nyumba yake. Na baada yake Shemaya mwana wa Shekania, mlinzi wa lango la mashariki, akajenga. 30 Baada yake Hanania, mwana wa Shelemia, na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, wakajenga sehemu nyingine. Meshulamu mwana wa Berekia akajenga kuelekea kwenye vyumba vyake. 31 Baada yake Malkiya, mmoja wa wafua dhahabu, akajenga mpaka nyumba ya watumishi wa hekalu na wafanyabiashara waliokuwa wakielekea lango la gereza na mpaka chumba cha juu cha pembeni. 32 Wafanyabiashara wa dhahabu na wafanyabiashara walijenga kati ya chumba cha juu cha kona na Lango la Kondoo.
<- Nehemia 2Nehemia 4 ->