1 Baada ya mambo haya, Yesu alienda pande za Bahari ya Galilaya, pia huitwa Bahari ya Tiberia. 2 Mkutano mkubwa ulikuwa ukimfuata kwa sababu waliona ishara alizozifanya kwa waliokuwa wagonjwa. 3 Yesu alipanda juu hadi upande wa juu wa mlima na akakaa huko na wanafunzi wake 4 (Na Pasaka, Sikukuu ya Wayahudi ilikuwa imekaribia). 5 Yesu alipoinua macho yake juu na kuona umati mkubwa unakuja kwake, akamwambia Filipo, “Tutakwenda wapi kununua mikate ili hawa waweze kula”? 6 (Lakini Yesu aliyasema haya kwa Filipo kwa kumjaribu kwa kuwa yeye mwenyewe alijua atakachofanya). 7 Filipo akamjibu, “Hata mikate ya thamani ya dinari mia mbili isingelitosha hata kila mmoja kupata hata kipande kidogo.” 8 Andrea, mmoja wa wanafunzi wake ndugu yake Simoni Petro akamwambia 9 Yesu, “Kuna mvulana hapa ana mikate mitano na samaki wawili, lakini hii yafaa nini kwa watu wengi namna hii?” 10 Yesu akawambia, “Waketisheni watu chini” (kulikuwa na nyasi nyingi mahali pale). Hivyo wanaume wapata elfu tano wakakaa chini. 11 Kisha Yesu akachukua ile mikate mitano akashukuru akawawagawia wale waliokuwa wamekaa. Vivyo hivyo akawagawia samaki kwa kadiri ya vile wavyohitaji. 12 Watu waliposhiba, aliwambia wanafunzi wake, “Vikusanyeni vipande vya mabaki, vilivyobaki ili kwamba kisipotee chochote.” 13 Basi wakakusanya na kujaza vikapu kumi na viwili, vipande vya mikate mitano ya shayiri- vipande vilivyosazwa na wale waliokula. 14 Kisha watu walipoona ishara hii aliyoifanya walisema, “Kweli huyu ndiye yule nabii ajaye ulimwenguni.” 15 Yesu alipotambua kuwa walikuwa wanataka kumkamata ili wamfanye kuwa mfalme wao, alijitenga, tena na akaenda mlimani yeye peke yake. 16 Ilipokuwa jioni, wanafunzi wake walishuka kwenda ziwani. 17 Wakapanda kwenye mtumbwi na walikuwa wakivuka kuelekea Kapernaumu. (Giza lilikuwa limeingia na Yesu alikuwa bado hajaja kwao). 18 Wakati huo upepo mkali ulikuwa ukivuma, na bahari ilikuwa ikendelea kuchafuka. 19 Tena wanafunzi wake walipokuwa wamepiga makasia kama ishirini na matano au thelathini, wakamwona Yesu akitembea juu ya bahari kuukaribia mtumbwi, na wakaogopa. 20 Lakini akawambia, “Ni mimi! Msiogope.” 21 Tena walikuwa tayari kumbeba kwenye mtumbwi, na mara mtumbwi ulifika kwenye nchi mahali walipokuwa wakienda. 22 Siku iliyofuata, mkutano uliokuwa umesimama upande wa bahari waliona kuwa hakuna mtumbwi mwingine isipokuwa ule ambayo Yesu na wanafunzi wake walikuwa hawajaupanda lakini wanafunzi wake walikuwa wameenda zao wenyewe. 23 (Ingawa, kulikuwa na baadhi ya mitumbwi iliyotoka Tiberia karibu na mahali walipokula mikate baada ya Bwana kutoa shukrani). 24 Wakati makutano walipotambua kuwa sio Yesu wala wanafunzi wake walikuwa kule, wao wenyewe walipanda ndani ya mitumbwi wakaenda Kapernaumu wakimtafuta Yesu. 25 Baada ya kumpata upande mwingine wa ziwa wakamuuliza, “Rabbi ulikuja lini huku?” 26 Yesu akawajibu, akawambia, Amini, amini, mnanitafuta mimi, sio kwa sababu mliziona ishara, bali kwa sababu mlikula mikate na kushiba. 27 Acheni kukifanyia kazi chakula chenye kuharibika, bali mkifanyie kazi chakula kidumucho hata milele kile ambacho mwana wa Adamu atawapa, kwa kuwa Mungu Baba ameweka muhuri juu yake.” 28 Kisha wakamwambia, “Ni nini tunapaswa kufanya ili kuzifanya kazi za Mungu?” 29 Yesu akajibu, “Hii ndiyo kazi ya Mungu: kwamba mmwamini yeye aliyemtuma.” 30 Basi wakamwambia, “Ni ishara zipi utakazofanya, kwamba tunaweza kuziona na kukuamini? Utafanya nini? 31 Baba zetu walikula manna jangwani, kama ilivyo andikwa, “Aliwapa mikate kutoka mbinguni ili wale.” 32 Kisha Yesu akawajibu, “Amini, amini, sio Musa aliyewapa mkate kutoka mbinguni, bali Baba yangu ndiye awapaye mkate wa kweli kutoka mbinguni. 33 Kwa kuwa mkate wa Mungu ni ule ushukao kutoka mbinguni na kuupatia uzima ulimwengu. 34 Basi wakamwambia, “Bwana tupatie huu mkate wakati wote.” 35 Yesu akawambia, “Mimi ndiye mkate wa uzima, yeye ajaye kwangu hatapata njaa na yeye aniaminiye hatahisi kiu kamwe.” 36 Ingawa niliwaambia kwamba, mmeniona, na bado hamuamini. 37 Wote ambao Baba anaonipa watakuja kwangu, na yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kabisa. 38 Kwa kuwa nimeshuka kutoka mbinguni, sio kwa ajili ya kufanya mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenituma. 39 Na haya ndiyo mapenzi yake aliyenituma, kwamba nisimpoteze hata mmoja wa wale alionipa, bali nitawafufua siku ya mwisho. 40 Kwa kuwa haya ndiyo mapenzi ya Baba yangu, kwamba yeyote amtazamaye Mwana na kumwamini apate uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho. 41 Kisha wayahudi wakamnung`unikia kumhusu yeye kwa sababu alisema, “Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni.” 42 Wakasema, “Huyu siyo Yesu mwana wa Yusuph, ambaye baba yake na mama yake tunamfahamu? Imekuwaje sasa anasema, 'Nimeshuka kutoka mbinguni`?” 43 Yesu akajibu, akawambia, “Msinung'unikiane miongoni mwenu wenyewe. 44 Hakuna mtu ajaye kwangu asipovutwa na Baba yangu aliyenituma, nami nitamfufua siku ya mwisho. 45 Kwa kuwa imeandikwa katika manabii, 'Watafundishwa na Mungu.' Kila aliyesikia na amejifunza kutoka kwa Baba, huja kwangu. 46 Sio kwamba kuna mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yeye atokaye kwa Mungu- amemwona Baba. 47 Amini, amini yeye aaminiye anao uzima wa milele. 48 Mimi ni mkate wa uzima. 49 mababa zenu walikula manna jangwani, na wakafa. 50 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, ili kwamba mtu aule sehemu yake ili asife. 51 Mimi ni mkate uishio ambao umeshuka kutoka mbinguni. Kama mtu yeyote akila sehemu ya mkate huu, ataishi milele. Mkate nitakao utoa ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.” 52 Wayahudi wakakasirika wenyewe kwa wenyewe na wakaanza kubishana wakisema, “Mtu huyu anawezaje kutupa mwili wake tuule?” 53 Kisha Yesu akawambia, “Amini, amini, msipoula mwili wa Mwana wa Adamu na kuinywa damu yake, hamta kuwa na uzima ndani yenu. 54 Yeyote aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele, nami nitamfufua siku ya mwisho. 55 Kwa kuwa mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. 56 Yeye aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu, nami ndani yake. 57 Kama Baba mwenye uzima alivyonituma, na kama niishivyo kwa sababu ya Baba, na yeye pia ataishi kwa sababu yangu. 58 Huu ndio mkate ushukao kutoka mbinguni, sio kama vile mababa walivyo kula wakafa. Yeye aulaye mkate huu ataishi milele. 59 Yesu aliyasema mambo haya ndani ya sinagogi alipokuwa akifundisha huko Kapernaumu. 60 Ndipo wengi wa wanafunzi wake waliposikia haya, wakasema, “Hili nifundisho gumu ni nani awezaye kulipokea?” 61 Yesu kwa sababu alijua ya kuwa wanafunzi wake walikuwa wakilinung'unikia jambo hili, akawambia je jambo hili linawakwaza? 62 Basi itakuaje mtakapomwona mwana wa Adamu akishuka kutoka alikokuwa kabla? 63 Ni Roho ndiye atoaye uzima. Mwili haufaidii kitu chochote. Maneno niliyoyasema kwenu ni roho na ni uzima. 64 Bado kuna watu kati yenu wasioamini.” kwa sababu Yesu alijua tangu mwanzo yule ambaye asiyeweza kuamini na yeye ambaye angemsaliti. 65 Akawambia, ni kwa sababu hii niliwambia kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amepewa na Baba.” 66 Baada ya haya wanafunzi wake wengi walirudi nyuma na hawakuambatana naye tena. 67 Yesu akawambia wale kumi na wawili, “Je na ninyi mnataka kuondoka?” 68 Simoni Petro akamjibu, “Bwana twende kwa nani kwani wewe unayo maneno ya uzima wa milele, 69 na tumeamini na kujua kuwa wewe ni Mtakatifu wa Mungu.” 70 Yesu akawambia, “Je mimi sikuwachagua ninyi, na mmoja wenu ni ibilisi? 71 Sasa alikuwa akiongea kuhusu Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, kwa kuwa alikuwa ni yeye akiwa mmoja wa wale kumi na wawili, ambaye ndiye angemsaliti Yesu.
<- Yohana 5Yohana 7 ->