1 Ugonvi na migogoro miongoni mwenu vyatoka wapi? Haviinuki kutoka katika tamaa zenu mbaya zinazoleta vita ndani ya washirika wenu? 2 Mnatamani kile msichokuwa nacho. Mnauwa na mnafukuzia kile msichoweza kuwa nacho. Mnapigana na kugombana, na bado hampati kwa sababu hamumwombi Mungu. 3 Mnaomba na hampokei kwa sababu mnaomba kwa ajili ya mambo mabaya, ili kwamba muweze kuvitumia kwa tamaa zenu mbaya. 4 Enyi wazinzi! Hamjui kwamba urafiki na ulimwengu ni uadui dhidi ya Mungu? Kwa hiyo, yeyote aamuaye kuwa rafiki wa ulimwengu hujifanya mwenyewe adui wa Mungu. 5 Au mnadhani maandiko hayana maana yasemapo kwamba Roho aliyoweka ndani yetu ana wivu sana kwa ajili yetu? 6 Lakini Mungu hutoa neema zaidi, ndiyo maana maandiko husema, “Mungu humpinga mwenye kiburi, lakini humpa neema mnyenyekevu.” 7 Hivyo, jitoeni kwa Mungu. Mpingeni ibilisi na yeye atakimbia kutoka kwenu. 8 Sogeeni karibu na Mungu, na yeye atakaribia karibu nanyi. Safisheni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na takaseni mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. 9 Huzunikeni, ombolezeni, na kuria! Geuzeni kicheko chenu kuwa huzuni na furaha yenu kuwa maombolezo. 10 Jinyenyekezeni wenyewe mbele za Bwana, na atawainua juu. 11 Msineneane kinyume ninyi kwa ninyi, ndugu. Mtu anenaye kinyume na ndugu yake, au kumhukumu ndugu yake, hunena kinyume na sheria na huihukumu sheria ya Mungu. Mkiihukumu sheria, hamuitii sheria, bali mnaihukumu. 12 Ni mmoja tu ambaye ni mtoa sheria na hakimu, Mungu, yeye ambaye ana uwezo wa kuokoa na kuangamiza. Wewe ni nani ambaye unamhukumu jirani yako? 13 Sikilizeni, ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu, na kukaa mwaka huko, na kufanya biashara, na kutengeneza faida.” 14 Ni nani ajuaye nini kitatokea kesho, na maisha yenu ni nini hasa? Kwa kuwa mnafanana kama ukungu unaotokea kwa muda mfupi na kisha hupotea. 15 Badala yake mngesema, “kama ni mapenzi ya Bwana, tutaishi na tutafanya hiki au kile.” 16 Lakini sasa mnajivuna juu ya mipango yenu. Majivuno yote hayo ni uovu. 17 Kwahiyo, kwake yeye ajuaye kutenda mema lakini hayatendi, kwake huyo ni dhambi.
<- Waraka wa Yakobo 3Waraka wa Yakobo 5 ->