23
1 Sara akaishi mika mia moja na ishirini na saba. Hii ndiyo ilikuwa ni miaka ya maisha ya Sara. 2 Sara akafa katika Kiriathi Arba, ambayo ni Hebroni, katika nchi ya Kanaani. Abraham akaomboleza na kumlilia Sara. 3 Kisha Abraham akainuka na kutoka kwa mkewe aliye kufa, akanena na watoto wa kiume wa Hethi, akisema, 4 “Mimi ni mgeni kati yenu. Tafadhari nipatieni mahali pa kuzikia miongoni mwenu, ili kwamba niweze kuzika wafu wangu.” 5 Wana wa Hethi wakamjibu Abraham, wakasema, 6 “Tusikilize, bwana wangu. Wewe ni mwana wa Mungu miongoni mwetu. Zika wafu wako katika makaburi yetu utakayochagua. Hakuna miongoni mwetu atakaye kuzuilia kaburi lake, kwa ajili ya kuzikia wafu wako.” 7 Abraham akainuka na kusujudu chini kwa watu wa nchi ile, kwa wana wa Hethi. 8 Akawaambia, akisema, “ikiwa mmekubali mimi kuzika wafu wangu, ndipo nisikilizeni, msihini Efroni mwana wa Sohari kwa ajili yangu. 9 Mwambieni aniuzie pango la Makpela, ambalo analimiliki, ambalo liko mwishoni mwa shamba lake. Kwa bei kamili aniuzie waziwazi mbele ya watu kama miliki ya kuzikia.” 10 Efroni alikuwa ameketi miongoni mwa wana wa Hethi, hivyo Efroni Mhiti akamjibu Abraham alipowasikia wana wa Hethi, wote ambao walikuwa wamekuja langoni mwa mji wake, akasema, 11 “Hapana, bwana wangu, nisikilize. Ninakupatia shamba na pango ambalo limo ndani yake. Ninakupatia mbele ya wana wa watu wangu. Ninakupatia uzike wafu wako.” 12 Kisha Abraham akasujudu chini mbele ya watu wa nchi ile. 13 Akamwambia Efroni watu wa nchi ile wakisikiliza, akasema, ikiwa uko radhi, tafadhari nisikilize. Nitalipia shamba. Chukua fedha kwangu, na nitazika wafu wangu pale.” 14 Efroni akamjibu Abraham, akisema, 15 “Tafadhari bwana wangu, nisikilize. Kipande cha ardhi kinathamani ya shekeli mia nne za fedha, na hiyo ni kitu gani kati yangu mimi na wewe? wazike wafu wako.” 16 Abraham akamsikiliza Efroni na akampimia Efroni kiwango cha fedha alizosema mbele ya wana wa Helthi wakisikiliza, shekeli mia nne za fedha, kwa mujibu wa viwango vya vipimo vya kibiashara. 17 Kwa hiyo shamba la Efroni, lililokuwa katika Makpela, mbele ya Mamre, shamba pamoja na pango lililokuwamo ndani yake na miti yote iliyokuwamo ndani ya shamba na iliyokuwa mpakani ikatolewa 18 kwa Abraham kwa njia ya manunuzi mbele ya wana wa Hethi, na mbele ya wote waliokuja malangoni pa mji wake. 19 Baada ya haya, Abraham akamzika Sara mkewe katika pango la shamba la Makpela, lililo mbele ya Mamre, ambayo ni Hebroni, katika nchi ya Kanaani. 20 Kwa hiyo shamba pamoja na pango likatolewa na wana wa Hethi kwa Abraham kama milki na eneo la kuzikia.
<- Mwanzo 22Mwanzo 24 ->
Mwanzo