Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
12
1 Katika kipindi hicho, Mikaeli, jemedari mkuu ambaye huwalinda watu wako, atainuka. Kutakuwa na wakati wa mateso ambao haujawahi kutokea tangu mwanzo wa taifa lolote mpaka kipindi hicho. Katika muda huo watu wako wataokolewa, yeyote ambaye jina lake litapatikana katika kitabu. 2 Na wengi wa wale waliolala katika mavumbi ya dunia watainuka. baadhi kwa uzima wa milele na baadhi kwa ajili ya fedheha na matwezo ya milele. 3 Wale wenye hekima watang'ara kama mng'ao wa anga la juu, na wale wenye kuwaelekeza wengine katika haki, watakuwa kama nyota milele na milele. 4 Lakini wewe, Danieli, yafunge maneno haya; kihifadhi kitabu kikiwa kimetiwa chapa mpaka nyakati za mwisho. Watu wengi watakimbia huku na kule, na maarifa yataongezeka. 5 Kisha mimi, Danieli, nilitazama, na kulikuwa na malaika wengine wawili wamesimama. Mmoja alisimama katika upande huu wa ukingo wa mto, na mwingine alisimama katika ukingo wa upande mwingine wa mto. 6 Mmoja wao alimwambia mtu aliyevaa nguo za kitani, yeye aliyekuwa juu ya mkondo wa mto, “Je itachukua muda gani mpaka mwisho wa matukio haya ya kushangaza?” 7 Nilimsikia mtu yule aliyevaa nguo za kitani, aliyekuwa juu katika mkondo wa mto, aliinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni na kuapa kwa yeye aishiye milele kwamba itakuwa kwa wakati, nyakati, na nusu wakati. Na wakati nguvu za watu watakatifu zitakapokuwa zimeshaharibiwa, mambo haya yote yatakuwa yamemalizika. 8 Nilisikia, lakini sikufahamu. Basi nikamwuliza, “Bwana wangu, mambo haya yote yatakuwa na matokeo gani?” 9 Alisema, “Nenda zako Danieli, kwa kuwa maneno yamefungwa na kutiwa chapa mpaka wakati wa mwisho. 10 Watu wengi watakuwa wametakaswa, wameoshwa, na kusafishwa, lakini waovu wataenenda katika uovu. 11 Katika muda ule ambapo sadaka ya kawaida ya kuteketezwa itakapokuwa imeondolewa na chukizo la uharibifu liliosababisha ukiwa limesimamishwa, kutakuwa na siku zipatazo 1, 290. 12 Ana heri mtu yule anayengojea mpaka mwisho wa siku 1, 335. 13 Unapaswa uondoke uende njia yako hata mwisho, na kisha utapumzika. Utainuka katika sehemu uliyopewa, mwishoni mwa siku.”

<- Danieli 11
  • Danieli