17
1 Eliyas Mtishibi, kutoka Tishibi ya Gileadi, akamwambia Ahabu, “Kama BWANA, Mungu wa Israeli aishivyo, ambaye ninasimama, hakutakuwa na umande wala mvua isiipokuwa kwa neno langu.” 2 Kisha nenola BWANA, likammjia Eliya, likisema, 3 “Ondoka hapa uende mashariki; ukajifiche karibu na kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yorodani. 4 Nawe utakunywa maji ya kijito, na nimewaamuru kunguru kukulisha mahali hapo.” 5 Kwa hiyo Eliya akaenda kama neno la BWANA lilivyomwamuru. Akaenda kuishi karibu na kijito cha Kerithi, mashariki mwa Yorodani. 6 Nao kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, naye akanywa maji ya kijito kile. 7 Lakini baada ya muda kile kijito kikakauka kwa sababu hapakuwepo na mvua katika nchi. 8 Neno la BWANA likamjia, likisema, 9 “Inuka, uende Sarepta, ambao ni mji wa Sidoni, na ukaishi huko. Tazama nimemmwamuru mjane kukulisha.” 10 Kwa hiyo akainuka na akaenda Sarepta, na alipofika kwenye lango la mji, kulikuwa na mjane akiokota kuni. Kwa hiyo akamwita na akamwambia, “Tafadhali niletee maji kidogo kwenye jagi ninywe.” 11 Naye alipokuwa akienda kuleta maji alimwita, akamwambia, “tafadhali uniletee na kipande cha mkate mkononi.” 12 Naye akamjibu, “Kama BWANA Mungu wako aishivyo, sina mkate wowote, bali konzi moja ya unga katika chombo na mafuta kidogo kwenye chupa. Tazama, ninaokota kuni mbili ili niende kupika kwa ajili yangu na mwanangu, ili tule, na tusubiri kufa.” 13 Eliya akamwambia, “Usiogope. Nenda ukafanye kama usemavyo. lakini nitengenezee kwanza mimi na uniletee. Ndipo baadaye ujitenegenezee wewe na mwanao. 14 Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli anasema 'Lile pipa la unga halitaisha, wala ile chupa ya mafuta kukoma kutoa mafuta, mpaka siku ile BWANA atakapotuma mvua duniani.” 15 Kwa hiyo yule mjane akafanya kama Eliya alivyomwelekeza, yeye, na Eliya, na mwanae wakala kwa siku nyingi. 16 Lile pipa la Unga halikuisha, wala ile chupa ya mafuta haikukoma kutoa mafuta, kama vile neno la BWANA lilivyosema, kupitia kinywa cha Eliya. 17 Baada ya hayo mambo, yule mwana wa yule mwanamke, yule mwanamke mwenye nyumba, aliugua. Ugonjwa wake ukazidi hata akaishiwa pumzi kabisa. 18 Kwa hiyo mama yake akamwambia Eliya, “Je, una nini nami, ewe mtu wa Mungu? Je, umekuja kwangu ili kunikumbusha dhambi zangu na kumwua mwanangu?” 19 Naye Eliya akamjibu, “Nipe hapa mwanao.” Akambeba mtoto mikononi mwake na akampeleka mpaka chumbani alimokuwa akikaa, akamlaza yule mtoto kitanadani pake mwenyewe. 20 Akamlilia BWANA akisema, “BWANA Mungu wangu, kwa nini umeleta majanga kwa mjane ambaye mimi ninakaa, kwa kumwua mwanae?” 21 Kisha Eliya akajinyosha mwenyewe juu ya mtoto mara tatu; akamlilia BWANA akisema, “BWANA Mungu wangu, Ninakuomba, tafadhali uhai wa mtoto huyu umrudie.” 22 BWANA akaisikiliza sauti ya Eliya; uhai wa mtoto ukamrudia, na akawa hai. 23 Eliya akamchukua mtoto na akamtoa toka chumbani kwake akamleta kwenye ile nyumba; akampatia mama yake yule mtoto na akasema, “Tazama, mwanao yuko hai.” 24 Yule mwanamke akamwambia Eliya, “Sasa natambua kuwa wewe ni mtu wa Mungu, na kwamba neno la BWANA kinywani mwako ni la kweli.”
<- 1Wafalme 161Wafalme 18 ->
1Wafalme