4 Kisha neno la Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni likanijia kusema: 5 “Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu? 6 Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu? 7 Je, haya sio maneno ya Mwenyezi Mungu aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefela[a] zikiwa zimekaliwa na watu?’ ”
8 Neno la Mwenyezi Mungu likamjia tena Zekaria: 9 “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Fanyeni hukumu za haki, onesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi. 10 Msimdhulumu mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
11 “Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao. 12 Wakaifanya mioyo yao migumu kama gumegume, na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni aliyatuma kwa Roho wake Mtakatifu kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, alikasirika sana.
13 “ ‘Nilipoita, hawakusikiliza; kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. 14 ‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’ ”
<- Zekaria 6Zekaria 8 ->- a au upande wa magharibi chini ya vilima
Languages