Zaburi 57
Kuomba msaada
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu”. Utenzi wa Daudi. Baada ya kumponyoka Sauli pangoni.
1 Unihurumie, Ee Mungu, unihurumie,
kwa maana nafsi yangu inakukimbilia.
Chini ya uvuli wa mabawa yako nitakimbilia
hadi maafa yapite.
2 Namlilia Mungu Aliye Juu Sana,
Mungu anayetimiza makusudi yake kwangu.
3 Hutumana msaada kutoka mbinguni na kuniokoa,
akiwakemea wale wanaonifuatilia vikali;
Mungu huutuma upendo wake na uaminifu wake.
4 Niko katikati ya simba;
nimelala katikati ya wanyama wenye njaa kali,
watu ambao meno yao ni mikuki na mishale,
ambao ndimi zao ni panga kali.
5 Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
utukufu wako na uenee duniani kote.
6 Waliitegea miguu yangu nyavu,
nikachoshwa na dhiki.
Wamechimba shimo katika njia yangu,
lakini wametumbukia humo wao wenyewe.
7 Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti,
moyo wangu ni thabiti;
nitaimba na kusifu kwa nyimbo.
8 Amka, nafsi yangu!
Amka, kinubi na zeze!
Nitayaamsha mapambazuko.
9 Nitakusifu wewe, Ee Bwana, kati ya mataifa;
nitaimba habari zako, kati ya jamaa za watu.
10 Kwa maana upendo wako ni mkuu, waenea hadi mbinguni,
uaminifu wako unazifikia anga.
11 Ee Mungu, utukuzwe juu mbinguni,
Languages