1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene na yule Mariamu mwingine walienda kulitazama kaburi.
2 Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Mwenyezi Mungu alishuka kutoka mbinguni, akaenda kwenye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. 3 Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4 Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.
5 Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Isa aliyesulubiwa. 6 Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. 7 Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye anawatangulia kwenda Galilaya. Mtamwona huko.’ Sasa nimekwisha kuwaambia.”
8 Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, lakini wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. 9 Ghafula, Isa akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. 10 Ndipo Isa akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”
16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Isa alikuwa amewaagiza. 17 Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 Isa akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, nendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza[a] kwa Jina la Baba[b] na la Mwana[c] na la Roho[d] wa Mungu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
<- Mathayo 27- a Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali.
- b Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu.
- c Yaani Isa Al-Masihi, aliye na asili ya Mwenyezi Mungu, na uhusiano wa kipekee naye.
- d Ndiye anayefanya kazi ya Mwenyezi Mungu katika moyo wa mwanadamu, na kumshawishi nia yake kumfuata Isa Al-Masihi (Yohana 16:5-15).
Languages