3 Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku, 4 akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho. 5 Mimi na watu walio pamoja nami tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo awali, sisi tutawakimbia. 6 Watatufuatilia hadi tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia, 7 ninyi mtainuka mtoke mafichoni na kuuteka mji. Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atautia mkononi mwenu. 8 Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile Mwenyezi Mungu alivyoamuru. Tazameni, nimewaagiza.”
9 Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.
10 Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Yoshua akakusanya jeshi lake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawaongoza kwenda Ai. 11 Wanajeshi wote waliokuwa pamoja na Yoshua walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji. 12 Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka mafichoni kusubiri kushambulia, kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji. 13 Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.
14 Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na wanaume wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema kukutana na Israeli katika vita mahali palipotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji. 15 Yoshua na Waisraeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani. 16 Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji. 17 Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Waisraeli.
18 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai. 19 Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mafichoni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.
20 Wanaume wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani, lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wakiwakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao. 21 Basi Yoshua na Waisraeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kwenye mji, wakawageukia wanaume wa Ai na kuwashambulia. 22 Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka. 23 Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.
24 Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini. 25 Wanaume na wanawake elfu kumi na mbili waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai. 26 Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai. 27 Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amemwamuru Yoshua.
28 Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo. 29 Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo hadi jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe mengi makubwa juu yake, ambayo yamesalia hadi leo.
34 Hatimaye, Yoshua akasoma maneno yote ya sheria, yaani baraka na laana, kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Torati. 35 Hakuna neno lolote katika yale yote ambayo Musa alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakuwasomea kusanyiko lote la Waisraeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na wageni walioishi miongoni mwao.
<- Yoshua 7Yoshua 9 ->- a yaani sadaka za ushirika
Languages