6 “Kuweni hodari sana, kuweni waangalifu kutii yote yaliyoandikwa katika Kitabu cha Torati ya Musa, pasipo kugeuka upande wa kuume au kushoto. 7 Msishirikiane na mataifa yaliyobakia kati yenu, wala msiombe kwa majina ya miungu yao au kuapa kwayo. Msiitumikie wala kuisujudia. 8 Bali mtashikamana kwa uthabiti na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama vile mmefanya hadi sasa.
9 “Mwenyezi Mungu amewafukuza mbele yenu mataifa makubwa na yenye nguvu, hadi leo hakuna yeyote aliyeweza kusimama mbele yenu. 10 Mtu mmoja miongoni mwenu anafukuza watu elfu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapigania, kama alivyoahidi. 11 Kwa hiyo kuweni waangalifu sana kumpenda Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
12 “Lakini ikiwa mtageuka na kushikamana na mabaki ya mataifa haya yaliyosalia kati yenu na kama mtaoana na kushirikiana nao, 13 basi mwe na hakika kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa hayo mbele yenu. Badala yake, watakuwa tanzi na mitego kwenu, mijeledi migongoni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mwangamie kutoka nchi hii nzuri, ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa.
14 “Sasa mimi ninakaribia kwenda katika njia ya watu wote wa dunia. Mnajua kwa mioyo yenu na roho zenu kwamba hakuna ahadi zozote njema Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alizowaahidia, ambazo hazikutimia. Kila ahadi imetimizwa, hakuna hata moja ambayo haikutimia. 15 Lakini kama vile kila ahadi njema ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, imekuwa kweli, vivyo hivyo Mwenyezi Mungu ataleta maovu yote kama alivyoonya, hadi awe amewaangamiza kutoka nchi hii nzuri aliyowapa. 16 Mkilivunja agano la Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ambalo aliwaamuru ninyi, mkaenda na kuitumikia miungu mingine na kuisujudia, hasira ya Mwenyezi Mungu itawaka dhidi yenu, basi nanyi mtaangamia kutoka nchi nzuri aliyowapa ninyi.”
<- Yoshua 22Yoshua 24 ->
Languages