10 “Sasa basi, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoahidi, ameniweka hai kwa miaka arobaini na tano tangu alipomwambia Musa jambo hili, Waisraeli walipokuwa wanazunguka jangwani. Hivyo mimi hapa leo nina umri wa miaka themanini na tano! 11 Bado nina nguvu kama siku ile Musa aliponituma; nina nguvu za kwenda vitani sasa kama nilivyokuwa wakati ule. 12 Basi nipe nchi hii ya vilima, ambayo Mwenyezi Mungu aliniahidi siku ile. Wewe mwenyewe ulisikia wakati ule kwamba Waanaki walikuwa huko na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye ngome, lakini, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, nitawafukuza watoke huko kama vile alivyonena.”
13 Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune, na akampa Hebroni kama urithi wake. 14 Hivyo Hebroni imekuwa mali ya Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi tangu wakati ule, kwa sababu alimwandama Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wote. 15 (Hebroni uliitwa Kiriath-Arba hapo mwanzo, kuitanishwa na Arba aliyekuwa mtu mkuu kupita wote miongoni mwa Waanaki.)
Languages