7 “Basi hili ndilo Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Kwa nini kujiletea maafa makubwa kama haya juu yenu kwa kujikatilia mbali kutoka Yuda wanaume na wanawake, watoto na wanyonyao, hata kujiacha bila mabaki? 8 Kwa nini kuichochea hasira yangu kwa kazi ya mikono yenu, kuifukizia uvumba miungu mingine huko Misri, mahali mlipokuja kuishi? Mtajiangamiza wenyewe na kujifanya kitu cha kulaania na shutumu miongoni mwa mataifa yote duniani. 9 Je, mmesahau uovu uliotendwa na baba zenu, na wafalme na malkia wa Yuda, na uovu uliofanywa na ninyi na wake zenu katika nchi ya Yuda na barabara za Yerusalemu? 10 Hadi leo hawajajinyenyekeza au kuonesha heshima, wala hawajafuata sheria yangu na amri nilizoweka mbele yenu na baba zenu.
11 “Kwa hiyo, hili ndilo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli, asemalo: Mimi nimekusudia kuleta maafa juu yenu, na kuiangamiza Yuda yote. 12 Nitawaondoa mabaki ya Yuda waliokusudia kwenda Misri kukaa huko. Wote wataangamia huko Misri, wataanguka kwa upanga au kufa kwa njaa. Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana, watakufa kwa upanga au njaa. Watakuwa kitu cha kulaania na cha kutisha, cha laumu na shutumu. 13 Nitawaadhibu wanaoishi Misri kwa upanga, njaa na tauni kama nilivyoiadhibu Yerusalemu. 14 Hakuna hata mmoja wa mabaki ya Yuda ambaye ameenda kuishi Misri atakayeepuka au kunusurika ili kurudi katika nchi ya Yuda, ambayo wanaitamani sana kurudi na kuishi ndani yake, hakuna hata mmoja atakayerudi isipokuwa wakimbizi wachache.”
15 Kisha wanaume wote ambao walijua kwamba wake zao walikuwa wakifukiza uvumba kwa miungu mingine, pamoja na wanawake wote waliokuwako, yaani kusanyiko kubwa na watu wote walioishi nchi ya Misri na Pathrosi, wakamwambia Yeremia, 16 “Hatutausikiliza ujumbe uliotuambia katika jina la Mwenyezi Mungu! 17 Hakika tutafanya kila kitu tulichosema tutakifanya: Tutafukiza uvumba kwa Malkia wa Mbinguni na tutammiminia sadaka zetu za kinywaji kama sisi na baba zetu, wafalme na wakuu wetu tulivyofanya katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu. Wakati ule tulikuwa na chakula tele, tulikuwa matajiri wala hatukupata dhara lolote. 18 Lakini tangu tulipoacha kumfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni na kummiminia sadaka za kinywaji, hatupati chochote, na tumekuwa tukiangamizwa kwa upanga na njaa.”
19 Wanawake wakaongeza kusema, “Tulipomfukizia uvumba Malkia wa Mbinguni, na kummiminia sadaka zetu za kinywaji, je, waume zetu hawakujua kwamba tulikuwa tukitengeneza maandazi kwa mfano wake, na kummiminia yeye sadaka za kinywaji?”
20 Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake waliokuwa wakimjibu, 21 “Je, Mwenyezi Mungu hakukumbuka na kufikiri kuhusu uvumba uliofukizwa katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu na ninyi pamoja na baba zenu, wafalme wenu, maafisa wenu na watu wa nchi? 22 Mwenyezi Mungu alipokuwa hawezi kuendelea kuvumilia matendo yenu maovu na mambo ya machukizo mliyoyafanya, nchi yenu ilikuwa kitu cha kulaaniwa na kuachwa ukiwa pasipo wakazi, kama ilivyo leo. 23 Kwa sababu mmefukiza uvumba na kufanya dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, nanyi hamkumtii wala kufuata sheria yake au amri zake au maagizo yake, maafa haya yamekuja juu yenu, kama mnavyoona sasa.”
24 Kisha Yeremia akawaambia watu wote, pamoja na wanawake, “Sikieni neno la Mwenyezi Mungu, enyi watu wote wa Yuda mlioko Misri. 25 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, Mungu wa Israeli: Ninyi na wake zenu mmeonesha kwa matendo yenu kile mlichoahidi mliposema, ‘Hakika tutatimiza nadhiri tulizoziweka za kumfukizia uvumba na kummiminia sadaka za kinywaji Malkia wa Mbinguni.’
29 “ ‘Hii itakuwa ndiyo ishara kwenu kwamba nitawaadhibu mahali hapa, asema Mwenyezi Mungu, ili mpate kujua kuwa onyo langu la madhara dhidi yenu hakika litatimizwa.’ 30 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Nitamtia Farao Hofra mfalme wa Misri mikononi mwa adui zake wanaoutafuta uhai wake, kama nilivyomtia Sedekia mfalme wa Yuda mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, adui aliyekuwa akiutafuta uhai wake.’ ”
<- Yeremia 43Yeremia 45 ->
Languages