6 Baada ya siku arobaini, Nuhu akafungua dirisha alilokuwa amelifanya katika safina, 7 akamtoa kunguru, naye akawa akiruka kwenda na kurudi hadi maji yalipokwisha kukauka juu ya dunia. 8 Kisha akamtoa hua ili aone kama maji yameondoka juu ya ardhi. 9 Lakini hua hakupata mahali pa kutua, kwa kuwa maji yalienea juu ya uso wa dunia yote, kwa hiyo akarudi kwa Nuhu ndani ya safina. Nuhu akanyoosha mkono akamchukua yule hua, akamrudisha ndani ya safina. 10 Nuhu akangojea siku saba zaidi, kisha akamtoa tena hua kutoka safina. 11 Jioni hua aliporudi kwa Nuhu alikuwa amebeba jani bichi la mzeituni lililochumwa wakati ule ule katika mdomo wake! Ndipo Nuhu akajua ya kuwa maji yameondoka juu ya dunia. 12 Akangojea siku saba zaidi na akamtuma tena hua, lakini wakati huu hua hakurudi tena kwa Nuhu.
13 Kufikia siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa mia sita na moja (601) wa maisha ya Nuhu, maji yalikuwa yamekauka duniani. Kisha Nuhu akatoa kifuniko juu ya safina, akaona ya kuwa uso wa ardhi ulikuwa umekauka. 14 Kufikia siku ya ishirini na saba ya mwezi wa pili, dunia ilikuwa imekauka kabisa.
15 Ndipo Mungu akamwambia Nuhu, 16 “Toka katika safina, wewe na mkeo, na wanao na wake zao. 17 Utoe nje kila aina ya kiumbe hai aliye pamoja nawe, wakiwamo ndege, wanyama na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, ili wakazae, na kuongezeka na kuijaza tena dunia.”
18 Kwa hiyo Nuhu akatoka nje pamoja na mkewe, na wanawe na wake zao. 19 Wanyama wote na viumbe vyote vinavyotambaa ardhini, na ndege wote, kila kitu kinachoenda juu ya nchi, aina moja baada ya nyingine vikatoka katika safina.
Languages