5 Kisha akaniambia, “Mwanadamu, tazama kuelekea kaskazini.” Hivyo nikatazama na kwenye ingilio la kaskazini mwa lango la madhabahu, nikaona sanamu hii ya wivu.
6 Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, je, unaona yale wanayoyafanya: mambo ya kuchukiza kabisa ambayo nyumba ya Israeli wanayatenda hapa, yatakayonifanya niende mbali na mahali pangu patakatifu? Lakini utayaona mambo yanayochukiza hata zaidi.”
7 Kisha akanileta hadi ingilio la ukumbi. Nikatazama, nami nikaona tundu ukutani. 8 Akaniambia, “Mwanadamu, sasa toboa ukuta huu.” Ndipo nikatoboa ule ukuta, nikaona hapo pana mlango.
9 Naye akaniambia, “Ingia ndani, ukaone maovu na machukizo wanayofanya humu.” 10 Hivyo nikaingia ndani na kutazama. Nikaona kuta zote zimechorwa aina mbalimbali ya viumbe vinavyotambaa, na wanyama wanaochukiza, na sanamu zote za nyumba ya Israeli. 11 Mbele ya hizo kuta walisimama wazee sabini wa nyumba ya Israeli, naye Yaazania mwana wa Shafani alikuwa amesimama miongoni mwao. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi, na moshi wa harufu nzuri ya uvumba ulikuwa unapanda juu.
12 Akaniambia, “Mwanadamu, umeona wanayoyafanya wazee wa Israeli wakiwa gizani, kila mmoja kwenye mahali pa ibada pa sanamu yake? Wao husema, ‘Mwenyezi Mungu hatuoni, Mwenyezi Mungu ameiacha nchi.’ ” 13 Akasema tena, “Utawaona wakifanya mambo yaliyo chukizo zaidi.”
14 Ndipo akanileta kwenye ingilio la lango la kaskazini la nyumba ya Mwenyezi Mungu, nami nikaona wanawake wameketi hapo, wakimwombolezea Tamuzi. 15 Akaniambia, “Je, mwanadamu, unaliona hili? Utayaona mambo yanayochukiza hata zaidi.”
16 Ndipo akanileta hadi kwenye ukumbi wa ndani wa nyumba ya Mwenyezi Mungu, na katika ingilio la Hekalu, kati ya baraza na madhabahu, palikuwa na wanaume wapatao ishirini na watano. Walikuwa wamelipa kisogo Hekalu la Mwenyezi Mungu na kuelekeza nyuso zao upande wa mashariki, wakilisujudia jua upande wa mashariki.
17 Akaniambia, “Je, umeona hili mwanadamu? Je, ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda kufanya machukizo wanayoyafanya hapa? Je, ni lazima pia waijaze nchi dhuluma na kuendelea siku zote kunikasirisha? Watazame wanavyonibania pua kana kwamba ninanuka! 18 Kwa hiyo nitawaadhibu kwa hasira; sitawaonea huruma wala kuwarehemu. Hata wakipiga makelele masikioni mwangu, sitawasikiliza.”
<- Ezekieli 7Ezekieli 9 ->
Languages