17 Paulo akiwa Mileto, alituma mjumbe kwenda Efeso kuwaita wazee wa kundi la waumini waje wakutane naye. 18 Walipofika akawaambia, “Ninyi wenyewe mnajua jinsi nilivyoishi muda wote nilikuwa nanyi, tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa jimbo la Asia. 19 Nilimtumikia Bwana Isa kwa unyenyekevu wote na kwa machozi nikivumilia taabu na mapingamizi yaliyonipata kutokana na hila za Wayahudi. 20 Mnajua kwamba sikusita kuhubiri jambo lolote ambalo lingekuwa la kuwafaa ninyi, lakini nilifundisha hadharani na nyumba kwa nyumba. 21 Nimewashuhudia Wayahudi na Wayunani kwamba inawapasa kumgeukia Mungu kwa kutubu dhambi na kumwamini Bwana wetu Isa Al-Masihi.
22 “Nami sasa nimesukumwa na Roho wa Mungu, ninaenda Yerusalemu wala sijui ni nini kitakachonipata huko. 23 Ila ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu wa Mungu amenionya kuwa vifungo na mateso vinaningoja. 24 Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani kwangu, kama kuyamaliza mashindano na kukamilisha ile kazi Bwana Isa aliyonipa, yaani kazi ya kuishuhudia Injili ya neema ya Mungu.
25 “Nami sasa najua kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwenu niliowahubiria ufalme wa Mungu atakayeniona tena. 26 Kwa hiyo nawatangazia leo, sina hatia ya damu ya mtu yeyote. 27 Kwa kuwa sikusita kuwatangazia mapenzi yote ya Mungu. 28 Jilindeni nafsi zenu na mlilinde lile kundi lote ambalo Roho wa Mungu amewaweka ninyi kuwa waangalizi wake. Chungeni jumuiya ya waumini ya Mungu, aliowanunua kwa damu yake mwenyewe. 29 Najua kwamba baada yangu kuondoka, mbwa-mwitu wakali watakuja kati yenu, ambao hawatalihurumia kundi. 30 Hata kutoka miongoni mwenu watainuka watu na kuupotosha ukweli ili wawavute wanafunzi wawafuate. 31 Hivyo jilindeni! Kumbukeni kwamba kwa miaka mitatu sikuacha kamwe kuwaonya kila mmoja kwa machozi usiku na mchana.
32 “Sasa nawakabidhi kwa Mungu na kwa neno la neema yake, linaloweza kuwajenga na kuwapa ninyi urithi miongoni mwa wote ambao wametakaswa. 33 Sikutamani fedha wala dhahabu wala vazi la mtu yeyote. 34 Ninyi wenyewe mnajua kwamba mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami. 35 Katika kila jambo nimewaonesha kwamba kwa njia hii ya kufanya kazi kwa bidii imetupasa kuwasaidia wadhaifu, mkikumbuka maneno ya Bwana Isa mwenyewe jinsi alivyosema, ‘Ni heri kutoa kuliko kupokea.’ ”
36 Paulo alipomaliza kusema haya akapiga magoti pamoja nao wote akaomba. 37 Wote wakalia, wakamkumbatia Paulo na kumbusu. 38 Kilichowahuzunisha zaidi ni kwa sababu ya yale maneno aliyosema kwamba kamwe hawatauona uso wake tena. Wakaenda naye hadi kwenye meli.
<- Matendo Ya Mitume 19Matendo Ya Mitume 21 ->
Languages