4 Kwa maana, kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa Kuzimu[a] katika vifungo vya giza wakae humo hadi ije hukumu; 5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, lakini akamhifadhi Nuhu, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba; 6 kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu, na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu; 7 na kama alimwokoa Lutu, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu 8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku): 9 ikiwa hivyo ndivyo, basi Mwenyezi Mungu anajua jinsi ya kuwaokoa wamchao Mungu kutoka majaribu, na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu. 10 Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka.
13 Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki karamu pamoja nanyi. 14 Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara. Wao ni hodari kwa kutamani; ni wana wa laana! 15 Wameiacha njia iliyo nyoofu, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu. 16 Lakini kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, alipoongea kwa sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.
17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji, na ukungu unaopeperushwa na tufani. Giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao. 18 Kwa maana wao hunena maneno matupu ya kiburi. Nao wanavutia tamaa mbaya za asili ya mwili, ili kuwashawishi watu ambao wanajiondoa kutoka kwa wale wanaoishi katika hatia. 19 Wanawaahidi uhuru wakati wao wenyewe ni watumwa wa upotovu; kwa maana “mtu ni mtumwa wa chochote kinachomtawala.” 20 Kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Isa Al-Masihi, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya kuliko ile ya kwanza. 21 Ingekuwa afadhali kwao kama hawangeijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa. 22 Kwao mithali zimetukia kuwa za kweli, zinaposema: “Mbwa huyarudia matapiko yake mwenyewe,” tena, “Nguruwe aliyeoshwa hurudi kugaagaa matopeni.”
<- 2 Petro 12 Petro 3 ->- a Kuzimu hapa linalotokana na neno Tartarus la Kiyunani; maana yake ni kule ndani sana katika mahali pa mateso kwa watu waliopotea.
Languages