7 Lakini tunayo hazina hii katika vyombo vya udongo, ili ijulikane wazi kwamba uwezo huu wa ajabu unatoka kwa Mungu, wala si kwetu. 8 Twataabika kila upande lakini hatuangamizwi; twaona wasiwasi lakini hatukati tamaa; 9 twateswa lakini hatuachwi; twatupwa chini lakini hatupondwi. 10 Siku zote twachukua katika mwili kufa kwake Isa ili uzima wa Isa uweze kudhihirishwa katika miili yetu. 11 Kwa maana sisi tulio hai siku zote tumetolewa tufe kwa ajili ya Isa, ili uzima wake upate kudhihirishwa katika mwili wetu upatikanao na mauti. 12 Hivyo basi, mauti inatenda kazi ndani yetu, bali uzima unatenda kazi ndani yenu.
13 Imeandikwa, “Niliamini, kwa hiyo nimesema.” Kwa roho yule yule wa imani pia tuliamini na hivyo tunasema, 14 kwa sababu tunajua kwamba yeye aliyemfufua Bwana Isa kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia pamoja na Isa na kutuleta sisi pamoja nanyi mbele zake. 15 Haya yote ni kwa faida yenu, ili neema ile inavyowafikia watu wengi zaidi na zaidi ipate kusababisha shukrani nyingi kwa utukufu wa Mungu.
16 Kwa hiyo, hatukati tamaa. Ingawa utu wetu wa nje unachakaa, utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 17 Kwa maana dhiki yetu nyepesi iliyo ya kitambo inatutayarisha kwa ajili ya utukufu wa milele unaozidi kuwa mwingi kupita kiasi. 18 Kwa hivyo hatuangalii yale yanayoonekana, bali yale yasiyoonekana. Kwa maana yale yanayoonekana ni ya kitambo tu, bali yale yasiyoonekana ni ya milele.
<- 2 Wakorintho 32 Wakorintho 5 ->
Languages