2 Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na wapiganaji wake elfu tatu wa Israeli waliochaguliwa, ili kumtafuta Daudi huko. 3 Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko, 4 Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili.
5 Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali ambapo Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka.
6 Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?”
7 Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli.
8 Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome hadi ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.”
9 Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu na asiwe na hatia?” 10 Daudi akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, Mwenyezi Mungu mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au ataenda vitani na kuangamia. 11 Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.”
12 Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito.
13 Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima, mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao. 14 Daudi akapaza sauti kwa jeshi na kwa Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?”
15 Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako. 16 Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?”
17 Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?”
21 Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.”
22 Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua. 23 Mwenyezi Mungu humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. Mwenyezi Mungu alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa Mwenyezi Mungu. 24 Kwa hakika kama vile maisha yako yalivyokuwa ya thamani kwangu leo, vivyo hivyo maisha yangu na yawe na thamani kwa Mwenyezi Mungu na kuniokoa kutoka taabu zote.”
25 Ndipo Sauli akamwambia Daudi, “Mwanangu Daudi na ubarikiwe; utafanya mambo makubwa na hakika utashinda.”
Languages