6 Akajenga safu ya nguzo, yenye urefu wa dhiraa hamsini[d] na upana wa dhiraa thelathini. Mbele ya jengo hilo kulikuwa na baraza. Mbele ya baraza kulikuwa na nguzo na paa lililoning’inia.
7 Akajenga ukumbi wa kiti cha ufalme, yaani Ukumbi wa Hukumu, mahali ambapo angetolea hukumu, akaufunika kwa mbao za mwerezi kutoka sakafu hadi dari. 8 Jumba la kifalme ambamo angeishi, aliliweka nyuma kidogo, na lilijengwa kama jumba hilo la hukumu. Pia Sulemani akajenga jumba la kifalme lililofanana na hilo kwa ajili ya binti Farao, aliyekuwa amemwoa.
9 Majengo haya yote, kuanzia nje hadi kwenye ua mkuu, na kuanzia msingi hadi upenuni, yalijengwa kwa mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo kwa msumeno, na nyuso zake za ndani na za nje zililainishwa. 10 Misingi ilijengwa kwa mawe makubwa yaliyo bora, yenye urefu wa dhiraa kumi[e], na mengine urefu wa dhiraa nane[f]. 11 Sehemu za juu kulikuwa na boriti za mwerezi, na mawe yenye ubora wa hali ya juu, yaliyokatwa kwa vipimo. 12 Ule ua mkuu ulizungukwa na ukuta wa safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa, kama ulivyokuwa ua wa ndani wa Hekalu la Mwenyezi Mungu na baraza yake.
13 Mfalme Sulemani akatuma watu Tiro kumleta Hiramu[g], 14 ambaye mama yake alikuwa mjane kutoka kabila la Naftali na baba yake alikuwa mtu wa Tiro tena fundi wa shaba. Hiramu alikuwa na ustadi wa hali ya juu na mzoefu katika aina zote za kazi ya shaba. Alikuja kwa Mfalme Sulemani na kufanya kazi zake zote alizopangiwa.
15 Hiramu akasubu nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa dhiraa kumi na nane[h], na mzingo wa dhiraa kumi na mbili[i] kwa mstari. 16 Pia alitengeneza mataji mawili ya shaba ya kusubu ili kuyaweka juu ya hizo nguzo; kila taji lilikuwa na kimo cha dhiraa tano[j] kwenda juu. 17 Wavu wa mikufu iliyosokotewa kwenye zile taji juu ya zile nguzo, saba kwa kila taji. 18 Akatengeneza makomamanga katika safu mbili kuzunguka kila wavu kuremba mataji yaliyo juu ya nguzo. Alifanya hivyo kwa kila nguzo. 19 Mataji yaliyokuwa juu ya nguzo kwenye baraza, yalikuwa katika umbo la yungiyungi, kimo chake ni dhiraa nne[k]. 20 Juu ya mataji ya zile nguzo mbili, juu ya ile sehemu yenye umbo kama bakuli, karibu na ule wavu, kulikuwa na yale makomamanga mia mbili katika safu kuzunguka pande zote. 21 Hiramu akazisimamisha zile nguzo barazani pa Hekalu. Nguzo iliyokuwa upande wa kusini akaiita Yakini[l], na ile ya upande wa kaskazini akaiita Boazi[m]. 22 Mataji yaliyokuwa juu yalikuwa na umbo la yungiyungi. Hivyo kazi ya nguzo ikakamilika.
23 Hiramu akasubu Bahari ya chuma, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo, na kimo cha dhiraa tano. Mzunguko wake ulikuwa dhiraa thelathini. 24 Chini ya ukingo, ilizungukwa na mapambo ya maboga kumi kwa kila dhiraa. Maboga hayo yalikuwa yamesubiwa katika safu mbili ili kuwa kitu kimoja na hiyo Bahari.
25 Ile Bahari iliwekwa juu ya mafahali kumi na wawili, watatu wakielekea kaskazini, watatu wakielekea magharibi, watatu wakielekea kusini, na watatu wakielekea mashariki. Hiyo Bahari iliwekwa juu yao, na sehemu zao za nyuma zilielekeana. 26 Bahari hiyo ilikuwa na unene wa nyanda moja[n], na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi lililochanua; nayo ingejazwa na bathi elfu mbili[o].
27 Pia akatengeneza vitako kumi vya shaba vinavyoweza kuhamishika, kila kimoja kilikuwa na urefu wa dhiraa nne, upana dhiraa nne na kimo chake dhiraa tatu[p]. 28 Hivi ndivyo vile vitako vilivyotengenezwa: Vilikuwa na mbao za pembeni zilizounganishwa na mihimili. 29 Juu ya mbao kati ya hiyo mihimili kulikuwa na simba, mafahali na makerubi, pia kwenye mihimili yake. Juu na chini ya simba na mafahali kulikuwa na shada za maua yaliyofuliwa. 30 Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya kuyazungusha. Kila kitako kilikuwa na sinia iliyowekwa juu ya vishikizo vinne viliyosubiwa shada za maua kila upande. 31 Ndani ya kitako kulikuwa na nafasi ya wazi iliyokuwa na umbile la mviringo lenye kina cha dhiraa moja[q]. Nafasi hii ya wazi ilikuwa ya mviringo, pamoja na kitako chake ilikuwa dhiraa moja na nusu[r]. Kuzunguka huo mdomo wake kulitiwa nakshi. Papi za vitako zilikuwa mraba na si za mviringo. 32 Yale magurudumu manne yalikuwa chini ya papi, na vyuma vya kuyazungushia viliunganishwa kwenye kitako. Kipenyo cha kila gurudumu kilikuwa dhiraa moja na nusu. 33 Magurudumu hayo yalitengenezwa kama ya magari ya kukokotwa na farasi; vyuma vya kuzungushia magurudumu, duara zake, matindi yake na vitovu vyake, vyote vilikuwa vya kusubu.
34 Kila kitako kilikuwa na mikono minne, moja kwenye kila pembe, ukichomoza kutoka kile kitako. 35 Juu ya kitako kulikuwa na utepe wa mviringo wenye kina cha nusu dhiraa. Vishikio na papi vilishikamana upande wa juu wa kitako. 36 Aliweka nakshi za makerubi, simba na mitende juu ya vishikio na juu ya papi, katika kila nafasi, na shada za maua kuzunguka. 37 Hivi ndivyo Hiramu alivyotengeneza vile vitako kumi. Vyote vilisubiwa kwenye kalibu moja na vilifanana kwa vipimo na kwa umbo.
38 Kisha akatengeneza masinia kumi ya shaba, kila moja likiwa na ujazo wa bathi arobaini[s], yakiwa na kipenyo cha dhiraa nne[t] kila sinia moja kwa kila kimoja cha vile vitako kumi. 39 Aliweka vitako vitano upande wa kusini wa Hekalu na vingine vitano upande wa kaskazini. Akaweka ile Bahari upande wa kusini, katika pembe ya kusini-mashariki ya Hekalu. 40 Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia.
48 Sulemani pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu:
- a Dhiraa 100 ni sawa na mita 45.
- b Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5.
- c Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5.
- d Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5.
- e Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5.
- f Dhiraa nane ni sawa na mita 3.6.
- g au Huramu
- h Dhiraa 18 ni sawa na mita 8.1.
- i Dhiraa 12 ni sawa na mita 5.4.
- j Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25.
- k Dhiraa nne ni sawa na mita 1.8.
- l maana yake Atathibitisha
- m maana yake Imo nguvu
- n Nyanda moja ni sawa na sentimita 7.5.
- o Bathi 2,000 ni sawa na lita 40,000.
- p Dhiraa 3 ni sawa na mita 1.35.
- q Dhiraa moja ni sawa na sentimita 45.
- r Dhiraa moja na nusu ni sawa na sentimita 67.5.
- s Bathi 40 ni sawa na lita 800.
- t Dhiraa nne ni sawa na mita 1.8.
Languages