Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
10
Bwana Ataitunza Yuda
1 Mwombeni Bwana mvua wakati wa vuli;
ndiye Bwana atengenezaye mawingu ya tufani.
Huwapa watu manyunyu ya mvua,
pia mimea ya shambani kwa ajili ya kila mtu.
2 Sanamu huzungumza udanganyifu,
waaguzi huona maono ya uongo;
husimulia ndoto ambazo si za kweli,
wanatoa faraja batili.
Kwa hiyo watu wanatangatanga kama kondoo
walioonewa kwa kukosa mchungaji.
 
3 “Hasira yangu inawaka dhidi ya wachungaji,
nami nitawaadhibu viongozi;
kwa kuwa Bwana Mwenye Nguvu Zote
atalichunga kundi lake,
nyumba ya Yuda,
naye atawafanya kuwa kama farasi
mwenye kiburi akiwa vitani.
4 Kutoka Yuda litatokea Jiwe la pembeni,
kutoka kwake vitatoka vigingi vya hema,
kutoka kwake utatoka upinde wa vita,
kutoka kwake atatoka kila mtawala.
5 Kwa pamoja watakuwa kama mashujaa
wanaokanyaga barabara za matope
wakati wa vita.
Kwa sababu Bwana yu pamoja nao,
watapigana na kuwashinda wapanda farasi.
 
6 “Nitaiimarisha nyumba ya Yuda
na kuiokoa nyumba ya Yosefu.
Nitawarejesha kwa sababu
nina huruma juu yao.
Watakuwa kama watu ambao
sijawahi kuwakataa
kwa sababu mimi ndimi Bwana Mungu wao,
nami nitawajibu.
7 Waefraimu watakuwa kama mashujaa,
mioyo yao itafurahi kana kwamba ni kwa divai.
Watoto wao wataona na kufurahi,
mioyo yao itashangilia katika Bwana.
8 Nitawaashiria na kuwakusanya ndani.
Hakika nitawakomboa,
nao watakuwa wengi
kama walivyokuwa mwanzoni.
9 Ijapokuwa niliwatawanya miongoni mwa mataifa,
hata hivyo wakiwa katika nchi za mbali
watanikumbuka mimi.
Wao na watoto wao watanusurika katika hatari
nao watarudi.
10 Nitawarudisha kutoka Misri
na kuwakusanya toka Ashuru.
Nitawaleta katika nchi ya Gileadi na Lebanoni,
na hapo hapatakuwa na nafasi ya kuwatosha.
11 Watapita katika bahari ya mateso;
bahari iliyochafuka itatulizwa
na vilindi vyote vya Mto Naili vitakauka.
Kiburi cha Ashuru kitashushwa,
nayo fimbo ya utawala ya Misri itatoweka.
12 Nitawaimarisha katika Bwana,
na katika jina lake watatembea,”
asema Bwana.

<- Zekaria 9Zekaria 11 ->
  • Zekaria