Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
15
Usijipendeze Mwenyewe, Bali Wapendeze Wengine
1 Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe. 2 Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani. 3 Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.” 4 Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.

5 Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu, 6 ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Injili Sawa Kwa Wayahudi Na Kwa Watu Wa Mataifa
7 Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu. 8 Kwa maana nawaambia kwamba, Kristo amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonyesha kweli ya Mungu na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani, 9 pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa:
“Kwa hiyo nitakutukuza katikati ya watu wa Mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.”
10 Tena yasema,
“Enyi watu wa Mataifa, furahini
pamoja na watu wa Mungu.”
11 Tena,
“Msifuni Bwana, ninyi watu wa Mataifa wote,
na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”
12 Tena Isaya anasema,
“Shina la Yese litachipuka,
yeye atakayeinuka ili kutawala juu ya mataifa.
Watu wa Mataifa watamtumaini.”

13 Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.

Paulo Mhudumu Wa Watu Wa Mataifa
14 Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema na ufahamu wote, tena mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi. 15 Nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu kama kuwakumbusha tena kwa habari ya ile neema Mungu aliyonipa, 16 ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.

17 Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu. 18 Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya, 19 kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu. 20 Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine. 21 Lakini kama ilivyoandikwa:

“Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona,
nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”
22 Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.
Paulo Apanga Kwenda Rumi
23 Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi. 24 Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi mpaka huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo. 25 Sasa, niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko. 26 Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walioko miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu. 27 Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini. 28 Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania. 29 Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo.

30 Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo wa Roho Mtakatifu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu. 31 Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu, 32 ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi. 33 Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.

<- Warumi 14Warumi 16 ->
  • Warumi