Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
12
Mwanamke Na Joka
1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ukiwa chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake. 2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa. 3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake. 4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa. 5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanaume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi. 6 Yule mwanamke akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.
Malaika Mikaeli Amshinda Yule Joka
7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao. 8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa, na hapakuwa tena na nafasi yao huko mbinguni. 9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwengu wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.
Ushindi Mbinguni Watangazwa
10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:
“Sasa wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja
na mamlaka ya Kristo wake.
Kwa kuwa ametupwa chini
mshtaki wa ndugu zetu,
anayewashtaki mbele za Mungu
usiku na mchana.
11 Nao wakamshinda
kwa damu ya Mwana-Kondoo
na kwa neno la ushuhuda wao.
Wala wao hawakuyapenda maisha yao
hata kufa.
12 Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu
na wote wakaao humo!
Lakini ole wenu nchi na bahari,
kwa maana huyo ibilisi ameshuka kwenu,
akiwa amejaa ghadhabu,
kwa sababu anajua ya kuwa
muda wake ni mfupi!”

13 Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanaume. 14 Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko jangwani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu,*Maana yake ni miaka mitatu na nusu. ya wakati ambako yule joka hawezi kufika. 15 Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko. 16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake. 17 Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke na likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo.

<- Ufunuo 11Ufunuo 13 ->
  • Ufunuo
  • a