Zaburi 69
Kilio Cha Kuomba Msaada Wakati Wa Dhiki
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi.” Zaburi ya Daudi.
1 Ee Mungu, niokoe,
kwa maana maji yamenifika shingoni.
2 Ninazama kwenye vilindi vya matope,
pasipo mahali pa kukanyaga,
Nimefika kwenye maji makuu,
mafuriko yamenigharikisha.
3 Nimechoka kwa kuomba msaada,
koo langu limekauka.
Macho yangu yanafifia,
nikimtafuta Mungu wangu.
4 Wale wanaonichukia bila sababu
ni wengi kuliko nywele za kichwa changu;
wengi ni adui kwangu bila sababu,
wale wanaotafuta kuniangamiza.
Ninalazimishwa kurudisha
kitu ambacho sikuiba.
5 Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu,
wala hatia yangu haikufichika kwako.
6 Ee Bwana, ewe Bwana Mwenye Nguvu Zote,
wakutumainio wasiaibishwe
kwa ajili yangu;
wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu,
Ee Mungu wa Israeli.
7 Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako,
aibu imefunika uso wangu.
8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe.
9 Kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila,
matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.
10 Ninapolia na kufunga,
lazima nivumilie matusi.
11 Ninapovaa nguo ya gunia,
watu hunidharau.
12 Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga,
nimekuwa wimbo wa walevi.
13 Lakini Ee Bwana, ninakuomba,
kwa wakati ukupendezao;
katika upendo wako mkuu, Ee Mungu,
unijibu kwa wokovu wako wa hakika.
14 Uniokoe katika matope,
usiniache nizame;
niokoe na hao wanichukiao,
kutoka kwenye vilindi vya maji.
15 Usiache mafuriko yanigharikishe
au vilindi vinimeze,
au shimo lifumbe kinywa chake juu yangu.
16 Ee Bwana, unijibu, kwa wema wa upendo wako;
kwa huruma zako nyingi unigeukie.
17 Usimfiche mtumishi wako uso wako,
uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.
18 Njoo karibu uniokoe,
nikomboe kwa sababu ya adui zangu.
19 Unajua jinsi ninavyodharauliwa,
kufedheheshwa na kuaibishwa,
adui zangu wote unawajua.
20 Dharau zimenivunja moyo
na nimekata tamaa,
nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata,
wa kunituliza, lakini sikumpata.
21 Waliweka nyongo katika chakula changu
na walinipa siki nilipokuwa na kiu.
22 Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego,
nayo iwe upatilizo na tanzi.
23 Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,
nayo migongo yao iinamishwe daima.
24 Uwamwagie ghadhabu yako,
hasira yako kali na iwapate.
25 Mahali pao na pawe ukiwa,
wala asiwepo yeyote atakayeishi katika mahema yao.
26 Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi,
na kuzungumza juu ya maumivu ya wale uliowaumiza.
27 Walipize uovu juu ya uovu,
usiwaache washiriki katika wokovu wako.
28 Wafutwe kutoka kitabu cha uzima
na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.
29 Mimi niko katika maumivu na dhiki;
Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.
30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.
31 Hili litampendeza Bwana kuliko ngʼombe dume,
zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake.
32 Maskini wataona na kufurahi:
ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi!
33 Bwana huwasikia wahitaji
wala hadharau watu wake waliotekwa.
34 Mbingu na dunia zimsifu,
bahari na vyote viendavyo ndani yake,
35 kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni
na kuijenga tena miji ya Yuda.
Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki,
36 watoto wa watumishi wake watairithi
na wale wote walipendao jina lake