Zaburi 33
Ukuu Na Wema Wa Mungu
1 Mwimbieni Bwana kwa furaha, enyi wenye haki;
kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
2 Msifuni Bwana kwa kinubi,
mwimbieni sifa kwa zeze la nyuzi kumi.
3 Mwimbieni wimbo mpya;
pigeni kwa ustadi, na mpaze sauti za shangwe.
4 Maana neno la Bwana ni haki na kweli,
ni mwaminifu kwa yote atendayo.
5 Bwana hupenda uadilifu na haki;
dunia imejaa upendo wake usiokoma.
6 Kwa neno la Bwana mbingu ziliumbwa,
jeshi lao la angani kwa pumzi ya kinywa chake.
7 Ameyakusanya maji ya bahari
kama kwenye chungu;
vilindi vya bahari
ameviweka katika ghala.
8 Dunia yote na imwogope Bwana,
watu wote wa dunia wamche.
9 Kwa maana Mungu alisema, na ikawa,
aliamuru na ikasimama imara.
10 Bwana huzuia mipango ya mataifa,
hupinga makusudi ya mataifa.
11 Lakini mipango ya Bwana inasimama imara milele,
makusudi ya moyo wake kwa vizazi vyote.
12 Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
watu ambao aliwachagua kuwa urithi wake.
13 Kutoka mbinguni Bwana hutazama chini
na kuwaona wanadamu wote;
14 kutoka maskani mwake huwaangalia
wote wakaao duniani:
15 yeye ambaye huumba mioyo yao wote,
ambaye huangalia kila kitu wanachokitenda.
16 Hakuna mfalme aokokaye kwa ukubwa wa jeshi lake;
hakuna shujaa aokokaye kwa wingi wa nguvu zake.
17 Farasi ni tumaini la bure kwa wokovu,
licha ya nguvu zake nyingi, hawezi kuokoa.
18 Lakini macho ya Bwana yako kwa wale wamchao,
kwa wale tumaini lao liko katika upendo wake usio na kikomo,
19 ili awaokoe na mauti,
na kuwahifadhi wakati wa njaa.
20 Sisi tunamngojea Bwana kwa matumaini,
yeye ni msaada wetu na ngao yetu.
21 Mioyo yetu humshangilia,
kwa maana tunalitumainia jina lake takatifu.
22 Upendo wako usio na mwisho ukae juu yetu, Ee Bwana,