Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
Zaburi 3
Sala Ya Asubuhi Ya Kuomba Msaada
Zaburi ya Daudi. Alipomkimbia mwanawe Absalomu.
1 Ee Bwana, tazama adui zangu walivyo wengi!
Ni wengi kiasi gani wanaoinuka dhidi yangu!
2 Wengi wanasema juu yangu,
“Mungu hatamwokoa.”
 
3 Lakini wewe, Ee Bwana, ni ngao pande zote;
umeniwekea utukufu na kuinua kichwa changu.
4 Ninamlilia Bwana kwa sauti kuu,
naye ananijibu kutoka mlima wake mtakatifu.
 
5 Ninajilaza na kupata usingizi;
naamka tena, kwa maana Bwana hunitegemeza.
6 Sitaogopa makumi elfu ya adui,
wanaojipanga dhidi yangu kila upande.
 
7 Ee Bwana, amka!
Niokoe, Ee Mungu wangu!
Wapige adui zangu wote kwenye taya,
vunja meno ya waovu.
 
8 Kwa maana wokovu watoka kwa Bwana.
Baraka yako na iwe juu ya watu wako.

<- Zaburi 2Zaburi 4 ->
  • Zaburi