Zaburi 2
Mfalme Aliyechaguliwa Na Mungu
1 Kwa nini mataifa wanashauriana kufanya mabaya,
na kabila za watu kula njama bure?
2 Wafalme wa dunia wanajipanga
na watawala wanajikusanya pamoja
dhidi ya Bwana
na dhidi ya Mpakwa Mafuta wake.
3 Wanasema, “Tuvunje minyororo yao
na kuvitupilia mbali vifungo vyao.”
4 Yeye atawalaye mbinguni hucheka,
Bwana huwadharau.
5 Kisha huwakemea katika hasira yake
na kuwaogopesha katika ghadhabu yake, akisema,
6 “Nimemtawaza Mfalme wangu
juu ya Sayuni, mlima wangu mtakatifu.”
Ushindi Wa Mfalme
7 Nitatangaza amri ya Bwana:
Yeye aliniambia, “Wewe ni Mwanangu,
leo mimi nimekuzaa.
8 Niombe, nami nitayafanya mataifa
kuwa urithi wako,
miisho ya dunia kuwa milki yako.
9 Utawatawala kwa fimbo ya chuma
na kuwavunjavunja kama chombo cha mfinyanzi.”
10 Kwa hiyo, ninyi wafalme, kuweni na hekima;
mwonyeke, enyi watawala wa dunia.
11 Mtumikieni Bwana kwa hofu
na mshangilie kwa kutetemeka.
12 Mbusu Mwana, asije akakasirika
nawe ukaangamizwa katika njia yako,
kwa maana hasira yake inaweza kuwaka ghafula.