Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
Zaburi 142
Maombi Ya Kuokolewa Dhidi Ya Watesi
Utenzi wa Daudi. Alipokuwa pangoni. Maombi.
1 Namlilia Bwana kwa sauti,
nainua sauti yangu kwa Bwana anihurumie.
2 Namimina malalamiko yangu mbele zake,
mbele zake naeleza shida zangu.
 
3 Wakati roho yangu inapozimia ndani yangu,
wewe ndiwe unajua njia zangu.
Katika njia ninayopita
watu wameniwekea mtego.
4 Tazama kuume kwangu na uone,
hakuna hata mmoja anayejihusisha nami.
Sina kimbilio,
hakuna anayejali maisha yangu.
 
5 Ee Bwana, nakulilia wewe,
nasema, “Wewe ni kimbilio langu,
fungu langu katika nchi ya walio hai.”
6 Sikiliza kilio changu,
kwa sababu mimi ni mhitaji sana;
niokoe na wale wanaonifuatilia,
kwa kuwa wamenizidi nguvu.
7 Nifungue kutoka kifungo changu,
ili niweze kulisifu jina lako.
 
Ndipo wenye haki watanizunguka,
kwa sababu ya wema wako kwangu.

<- Zaburi 141Zaburi 143 ->
  • Zaburi