Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
Zaburi 137
Maombolezo Ya Israeli Uhamishoni
1 Kando ya mito ya Babeli tuliketi, tukaomboleza
tulipokumbuka Sayuni.
2 Kwenye miti ya huko
tulitundika vinubi vyetu,
3 kwa maana huko hao waliotuteka
walitaka tuwaimbie nyimbo,
watesi wetu walidai nyimbo za furaha;
walisema, “Tuimbieni wimbo mmoja kati ya nyimbo za Sayuni!”
 
4 Tutaimbaje nyimbo za Bwana,
tukiwa nchi ya kigeni?
5 Nikikusahau wewe, ee Yerusalemu,
basi mkono wangu wa kuume na usahau ujuzi wake.
6 Ulimi wangu ushikamane na kaakaa la kinywa changu
kama sitakukumbuka wewe,
kama nisipokufikiri Yerusalemu
kuwa furaha yangu kubwa.
 
7 Kumbuka, Ee Bwana, walichokifanya Waedomu,
siku ile Yerusalemu ilipoanguka.
Walisema, “Bomoa, Bomoa
mpaka kwenye misingi yake!”
 
8 Ee binti Babeli, uliyehukumiwa kuangamizwa,
heri yeye atakayekulipiza wewe
kwa yale uliyotutenda sisi:
9 yeye ambaye atawakamata watoto wako wachanga
na kuwaponda juu ya miamba.

<- Zaburi 136Zaburi 138 ->
  • Zaburi