Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
Zaburi 124
Shukrani Kwa Ukombozi Wa Israeli
Wimbo wa kwenda juu. Wa Daudi.
1 Kama Bwana asingalikuwa upande wetu;
Israeli na aseme sasa:
2 kama Bwana asingalikuwa upande wetu,
wakati watu walipotushambulia,
3 wakati hasira yao ilipowaka dhidi yetu,
wangalitumeza tungali hai,
4 mafuriko yangalitugharikisha,
maji mengi yangalitufunika,
5 maji yaendayo kasi
yangalituchukua.
 
6 Bwana asifiwe,
yeye ambaye hakuruhusu turaruliwe kwa meno yao.
7 Tumeponyoka kama ndege
kutoka mtego wa mwindaji;
mtego umevunjika,
nasi tukaokoka.
8 Msaada wetu ni katika jina la Bwana,
Muumba wa mbingu na dunia.

<- Zaburi 123Zaburi 125 ->
  • Zaburi