Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
4
Hekima Ni Bora Kupita Vitu Vyote
1 Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu;
sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.
2 Ninawapa mafundisho ya maana,
kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.
3 Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu,
ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,
4 baba alinifundisha akisema,
“Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote;
yashike maagizo yangu na wewe utaishi.
5 Pata hekima, pata ufahamu;
usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.
6 Usimwache hekima naye atakuweka salama;
mpende, naye atakulinda.
7 Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima.
Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.
8 Mstahi, naye atakukweza;
mkumbatie, naye atakuheshimu.
9 Atakuvika shada la neema kichwani mwako
na kukupa taji ya utukufu.”
 
10 Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia,
nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi.
11 Ninakuongoza katika njia ya hekima
na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka.
12 Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa;
ukimbiapo, hutajikwaa.
13 Mkamate sana elimu, usimwache aende zake;
mshike, maana yeye ni uzima wako.
14 Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu
wala usitembee katika njia ya watu wabaya.
15 Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo;
achana nayo, na uelekee njia yako.
16 Kwa kuwa hawawezi kulala mpaka watende uovu;
wanashindwa hata kusinzia mpaka wamwangushe mtu.
17 Wanakula mkate wa uovu,
na kunywa mvinyo wa jeuri.
 
18 Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko,
ambayo hungʼaa zaidi na zaidi mpaka mchana mkamilifu.
19 Lakini njia ya waovu ni kama giza nene;
hawajui kinachowafanya wajikwae.
 
20 Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia;
sikiliza kwa makini maneno yangu.
21 Usiruhusu yaondoke machoni pako,
yahifadhi ndani ya moyo wako;
22 kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata
na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.
23 Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo,
maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
24 Epusha kinywa chako na ukaidi;
weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.
25 Macho yako na yatazame mbele,
kaza macho yako moja kwa moja mbele yako.
26 Sawazisha mapito ya miguu yako
na njia zako zote ziwe zimethibitika.
27 Usigeuke kulia wala kushoto;
epusha mguu wako na ubaya.

<- Mithali 3Mithali 5 ->
  • Mithali