16 “ ‘Kuhani atamleta huyo mwanamke na kumsimamisha mbele za Bwana. 17 Kisha kuhani atachukua sehemu ya maji matakatifu ndani ya gudulia la udongo na kuchanganya na baadhi ya vumbi kutoka sakafu ya Maskani. 18 Baada ya kuhani kumsimamisha huyo mwanamke mbele za Bwana, atazifungua nywele za huyo mwanamke na kuweka sadaka ya ukumbusho mikononi mwake, ile sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu, huku kuhani mwenyewe akishikilia yale maji machungu yaletayo laana. 19 Kisha kuhani atamwapiza huyo mwanamke, akimwambia, “Ikiwa hakuna mwanaume mwingine aliyekutana kimwili nawe, wala hujapotoka na kuwa najisi wakati ukiwa umeolewa na mumeo, maji haya machungu yaletayo laana na yasikudhuru. 20 Lakini ikiwa umepotoka wakati ukiwa umeolewa na mume wako na umejinajisi mwenyewe kwa kukutana kimwili na mwanaume mwingine asiyekuwa mumeo”; 21 hapa kuhani atamweka huyo mwanamke chini ya laana ya kiapo akisema: “Bwana na awafanye watu wako wakulaani na kukukataa, wakati Bwana atakapolifanya paja lako kupooza na tumbo lako kuvimba. 22 Maji haya yaletayo laana na yaingie ndani ya mwili wako ili tumbo lako livimbe na paja lako lipooze.”[c]
23 “ ‘Kuhani ataandika laana hizi kwenye kitabu, kisha atazioshea laana hizo kwenye yale maji machungu. 24 Kuhani atamnywesha yule mwanamke yale maji machungu yaletayo laana, nayo maji haya yatamwingia na kumsababishia maumivu makali. 25 Kuhani atachukua sadaka ya nafaka kwa ajili ya wivu kutoka mikononi mwa huyo mwanamke, naye ataipunga mbele za Bwana na kuileta madhabahuni. 26 Kisha kuhani atachota sadaka ya nafaka mkono uliojaa kama sehemu ya kumbukumbu na kuiteketeza juu ya madhabahu, baada ya hayo, atamtaka huyo mwanamke anywe yale maji. 27 Kama amejitia unajisi na kukosa uaminifu kwa mumewe, wakati anapotakiwa anywe maji yale yaletayo laana, yatamwingia na kusababisha maumivu makali; tumbo lake litavimba na paja lake litapooza, naye atakuwa amelaaniwa miongoni mwa watu wake. 28 Hata hivyo, ikiwa huyo mwanamke hakujitia unajisi, naye ni safi, atasafishwa hatia na ataweza kuzaa watoto.
29 “ ‘Basi, hii ndiyo sheria ya wivu mwanamke anapopotoka na kujitia unajisi akiwa ameolewa na mumewe, 30 au hisia za wivu zinapomjia mwanaume kwa sababu ya kumshuku mkewe. Kuhani atamfanya huyo mwanamke kusimama mbele za Bwana na atatumia sheria hii yote kwa huyo mwanamke. 31 Mume atakuwa hana hatia ya kosa lolote, bali mwanamke atayachukua matokeo ya dhambi yake.’ ”
<- Hesabu 4Hesabu 6 ->