5 Ndipo kwa agizo la Bwana Mose akatoa amri ifuatayo kwa Waisraeli: “Kile wazao wa kabila la Yosefu wanachosema ni kweli. 6 Hivi ndivyo Bwana anavyoamuru kwa binti za Selofehadi: Wanaweza kuolewa na mtu yeyote wampendaye, mradi tu waolewe miongoni mwa koo za kabila za baba yao. 7 Hakuna urithi katika Israeli utakaohamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila Mwisraeli atatunza ardhi ya kabila lake aliyoirithi kutoka kwa baba zake. 8 Kila binti atakayerithi ardhi katika kabila lolote la Israeli ni lazima aolewe na mtu kutoka kabila na ukoo wa baba yake, ili kila Mwisraeli amiliki urithi wa baba zake. 9 Hakuna urithi uwezao kuhamishwa kutoka kabila moja kwenda kabila jingine, kwa kuwa kila kabila la Israeli litatunza nchi linayorithi.”
10 Kwa hiyo binti za Selofehadi wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Mose. 11 Binti za Selofehadi, ambao ni Mahla, Tirsa, Hogla, Milka na Noa, wakaolewa na waume, wana wa ndugu za baba yao. 12 Waliolewa ndani ya koo za wazao wa Manase mwana wa Yosefu, na urithi wao ukabaki katika ukoo na kabila la baba yao.