1 Baada ya Sabato, alfajiri mapema siku ya kwanza ya juma, Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikwenda kulitazama kaburi.
2 Ghafula, pakawa na tetemeko kubwa la ardhi, kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaenda penye kaburi, akalivingirisha lile jiwe na kulikalia. 3 Sura ya huyo malaika ilikuwa kama umeme, na mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji. 4 Wale walinzi wa kaburi walimwogopa sana, wakatetemeka hata wakawa kama wafu.
5 Yule malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope, kwa maana ninajua kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulubiwa. 6 Hayupo hapa, kwa kuwa amefufuka, kama vile alivyosema. Njooni mpatazame mahali alipokuwa amelazwa. 7 Kisha nendeni upesi mkawaambie wanafunzi wake kwamba, ‘Amefufuka kutoka kwa wafu, naye awatangulia kwenda Galilaya. Huko ndiko mtamwona. Sasa nimekwisha kuwaambia.’ ”
8 Hivyo wale wanawake wakaondoka pale kaburini wakiwa wamejawa na hofu, bali wakiwa na furaha nyingi. Wakaenda mbio kuwaeleza wanafunzi wake habari hizo. 9 Ghafula, Yesu akakutana nao, akasema, “Salamu!” Wale wanawake wakamkaribia, wakaishika miguu yake, wakamwabudu. 10 Ndipo Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.”
16 Basi wale wanafunzi kumi na mmoja wakaenda hadi Galilaya kwenye ule mlima ambao Yesu alikuwa amewaagiza. 17 Walipomwona, wakamwabudu; lakini baadhi yao wakaona shaka. 18 Yesu akawajia na kusema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. 19 Kwa sababu hii, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, 20 nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika mimi niko pamoja nanyi siku zote, hadi mwisho wa nyakati.”
<- Mathayo 27