5 Kisha akawauliza, “Kama mmoja wenu angekuwa na mtoto au ngʼombe wake aliyetumbukia katika kisima siku ya Sabato, je, hamtamvuta mara moja na kumtoa?” 6 Nao hawakuwa na la kusema.
12 Kisha Yesu akamwambia yule aliyewaalika, “Uandaapo karamu ya chakula cha mchana au cha jioni, usialike rafiki zako au ndugu zako au jamaa zako au majirani zako walio matajiri tu. Ukifanya hivyo, wao nao wanaweza kukualika kwao, nawe ukawa umelipwa kile ulichofanya na kupata thawabu yako. 13 Bali ufanyapo karamu, waalike maskini, vilema na vipofu, 14 nawe utabarikiwa kwa sababu hawa hawana uwezo wa kukulipa. Mungu atakulipa wakati wa ufufuo wa wenye haki.”
15 Mmoja wa wale waliokuwa pamoja naye mezani aliposikia hivi akamwambia Yesu, “Amebarikiwa mtu yule atakayekula katika karamu ya Ufalme wa Mungu!”
16 Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anaandaa karamu kubwa, akaalika watu wengi. 17 Wakati wa karamu ulipofika, akamtuma mtumishi wake akawaambie wale walioalikwa, ‘Karibuni, kila kitu ki tayari sasa.’
18 “Lakini wote, kila mmoja, wakaanza kutoa udhuru: Wa kwanza akasema, ‘Nimenunua shamba, lazima niende kuliona. Tafadhali niwie radhi.’
19 “Mwingine akasema, ‘Ndipo tu nimenunua jozi tano za ngʼombe wa kulimia, nami ninakwenda kuwajaribu, tafadhali niwie radhi.’ 20 Naye mwingine akasema, ‘Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.’
21 “Yule mtumishi akarudi, akampa bwana wake taarifa. Ndipo yule mwenye nyumba akakasirika, akamwagiza yule mtumishi wake, akisema, ‘Nenda upesi kwenye mitaa na vichochoro vya mjini uwalete maskini, vilema, vipofu na viwete.’
22 “Yule mtumishi akamwambia, ‘Bwana, yale uliyoniagiza nimefanya, lakini bado ipo nafasi.’
23 “Ndipo yule bwana akamwambia mtumishi wake, ‘Nenda kwenye barabara na vijia vilivyoko nje ya mji na uwalazimishe watu waingie ili nyumba yangu ipate kujaa. 24 Kwa maana nawaambia, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeionja karamu yangu.’ ”
25 Umati mkubwa wa watu ulikuwa ukisafiri pamoja na Yesu, naye akageuka, akawaambia, 26 “Mtu yeyote anayekuja kwangu hawezi kuwa mwanafunzi wangu kama hatanipenda mimi zaidi ya baba yake na mama yake, mke wake na watoto wake, ndugu zake na dada zake, naam, hata maisha yake mwenyewe. 27 Yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
28 “Ni nani miongoni mwenu ambaye kama anataka kujenga nyumba, hakai kwanza chini na kufanya makisio ya gharama aone kama ana fedha za kutosha kukamilisha? 29 La sivyo, akiisha kuweka msingi, naye akiwa hana uwezo wa kuikamilisha, wote waionao wataanza kumdhihaki, 30 wakisema, ‘Mtu huyu alianza kujenga lakini hakuweza kukamilisha.’
31 “Au ni mfalme gani atokaye kwenda kupigana vita na mfalme mwingine, ambaye hakai chini kwanza na kufikiri iwapo akiwa na jeshi la watu 10,000 ataweza kupigana na yule anayekuja na jeshi la watu 20,000? 32 Kama hawezi, basi wakati yule mwingine akiwa bado yuko mbali, yeye hutuma ujumbe wa watu na kuomba masharti ya amani. 33 Vivyo hivyo, yeyote miongoni mwenu ambaye hawezi kuacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
34 “Chumvi ni nzuri, lakini chumvi ikiwa imepoteza ladha yake, itafanywaje ili iweze kukolea tena? 35 Haifai ardhi wala kwa lundo la mbolea, bali hutupwa nje.