Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
16
Siku Ya Upatanisho
1 Bwana akasema na Mose baada ya kifo cha wale wana wawili wa Aroni waliokufa walipokaribia mbele za Bwana. 2 Bwana akamwambia Mose: “Mwambie ndugu yako Aroni asije wakati wowote atakavyo yeye ndani ya Patakatifu pa Patakatifu, nyuma ya pazia pale mbele ya kiti cha rehema kile kilichoko juu ya Sanduku la Agano, la sivyo atakufa, kwa sababu huwa ninatokea ndani ya wingu juu ya kile kiti cha rehema.

3 “Hivi ndivyo Aroni atakavyoingia katika mahali patakatifu: atachukua fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa. 4 Atavaa koti takatifu la kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani; atafunga mshipi wa kitani kiunoni, na kuvaa kilemba cha kitani. Haya ni mavazi matakatifu, kwa hiyo ni lazima aoge kwa maji kabla ya kuyavaa mavazi hayo. 5 Atachukua mbuzi dume wawili kutoka kwa jumuiya ya Israeli kwa ajili ya sadaka ya dhambi, na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.

6 “Aroni atamtoa huyo fahali kwa ajili ya sadaka yake ya dhambi ili afanye upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na nyumba yake. 7 Kisha atawachukua wale mbuzi dume wawili na kuwaleta mbele za Bwana kwenye ingilio la Hema la Kukutania. 8 Aroni atapiga kura kwa ajili ya hao mbuzi wawili, mmoja kwa ajili ya Bwana na mwingine kwa ajili ya kubebeshwa dhambi.*Yaani Azazeli, maana yake mbuzi wa ondoleo la dhambi; pia ms. 10, 26. 9 Aroni atamleta yule mbuzi ambaye kura ya Bwana imemwangukia na kumtoa dhabihu kwa ajili ya sadaka ya dhambi. 10 Lakini mbuzi aliyechaguliwa kwa kura kuwa wa kubebeshwa dhambi atatolewa akiwa hai mbele za Bwana, atumike kwa kufanya upatanisho kwa kumwacha aende jangwani akiwa amebebeshwa dhambi.

11 “Aroni atamleta yule fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake na nyumba yake, naye atamchinja huyo fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe. 12 Atachukua chetezo kilichojaa makaa yanayowaka kutoka madhabahuni mbele za Bwana, na konzi mbili za uvumba laini uliosagwa vizuri wenye harufu, na kuvipeleka nyuma ya pazia. 13 Ataweka uvumba juu ya moto mbele za Bwana, na moshi wa uvumba utafunika kile kiti cha rehema kilicho juu ya Ushuhuda, ili asife. 14 Atachukua sehemu ya damu ya fahali, na kwa kidole chake atanyunyiza sehemu ya mbele ya kiti cha rehema; kisha atanyunyiza sehemu ya hiyo damu kwa kidole chake mara saba mbele ya kiti cha rehema.

15 “Kisha atamchinja mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu, na kuichukua damu yake nyuma ya pazia, na aifanyie kama alivyofanya kwa damu ya fahali: Atanyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele yake. 16 Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu kwa sababu ya unajisi na uasi wa Waisraeli, kwa dhambi zao zozote. Atafanya hivyo kwa ajili ya Hema la Kukutania, ambalo liko miongoni mwao katikati ya unajisi wao. 17 Mtu yeyote haruhusiwi kuwa ndani ya Hema la Kukutania, kuanzia wakati Aroni anapoingia kufanya upatanisho katika Patakatifu pa Patakatifu, hadi atakapotoka nje, baada ya kujifanyia upatanisho yeye mwenyewe na nyumba yake, pamoja na jumuiya yote ya Israeli.

18 “Kisha atatoka aje kwenye madhabahu yaliyo mbele za Bwana na kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atachukua sehemu ya damu ya fahali na sehemu ya damu ya mbuzi, na kuiweka kwenye pembe za madhabahu. 19 Atanyunyiza baadhi ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.

20 “Aroni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai. 21 Aroni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, ili kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo. 22 Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote mpaka mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani.

23 “Kisha Aroni ataenda ndani ya Hema la Kukutania na kuvua yale mavazi ya kitani aliyoyavaa kabla ya kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu, naye atayaacha pale. 24 Ataoga kwa maji katika mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake ya kawaida. Kisha atatoka na kutoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yake na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya watu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mwenyewe, na kwa ajili ya watu. 25 Pia atachoma mafuta ya mnyama wa sadaka ya dhambi juu ya madhabahu.

26 “Yule mtu anayemwachia yule mbuzi wa kubebeshwa dhambi ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji; baadaye anaweza kuingia kambini. 27 Yule fahali na mbuzi waliotolewa kwa ajili ya sadaka za dhambi, ambao damu yao ilikuwa imeletwa Patakatifu pa Patakatifu kwa ajili ya kufanya upatanisho, ni lazima watolewe nje ya kambi. Ngozi zao, nyama, na matumbo pamoja na mavi vitateketezwa kwa moto. 28 Mtu atakayevichoma ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji; baadaye ataweza kuingia kambini.

29 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ni lazima mfunge, wala msifanye kazi yoyote, iwe mzawa au mgeni anayeishi miongoni mwenu, 30 kwa sababu siku hii upatanisho utafanyika kwa ajili yenu ili kuwatakasa. Kisha mtakuwa safi mbele za Bwana kutokana na dhambi zenu zote. 31 Ni Sabato ya mapumziko, na lazima mfunge; ni agizo la kudumu. 32 Kuhani ambaye ametiwa mafuta na kuwekwa wakfu ili kuingia mahali pa baba yake kama kuhani mkuu atafanya upatanisho. Atavaa mavazi matakatifu ya kitani, 33 na kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, na pia kwa ajili ya makuhani, pamoja na jumuiya yote ya watu.

34 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Upatanisho utafanywa mara moja tu kwa mwaka kwa ajili ya dhambi zote za Waisraeli.”

Ndivyo ilivyofanyika, kama vile Bwana alivyomwamuru Mose.

<- Mambo Ya Walawi 15Mambo Ya Walawi 17 ->
  • Mambo Ya Walawi
  • a