Link to home pageLanguagesLink to all Bible versions on this site
8
Mji Wa Ai Waangamizwa
1 Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake. 2 Utafanya Ai na mfalme wake kama ulivyofanya kwa mji wa Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kuchukua mateka wake na mifugo wake, kwa ajili yenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.”

3 Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua watu mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku 4 akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho. 5 Mimi na watu walio pamoja nami, tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutawakimbia. 6 Watatufuatilia mpaka tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia, 7 ninyi inawapasa mwinuke mtoke huko mafichoni na kuuteka mji. Bwana Mungu wenu atautia mkononi mwenu. 8 Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile Bwana alivyoamuru. Angalieni, nimewaagiza.”

9 Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.

10 Asubuhi na mapema siku iliyofuatia, Yoshua akawakutanisha watu wake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawa mbele ya watu kwenda Ai. 11 Watu wote wa vita waliokuwa pamoja naye walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji. 12 Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka katika uavizi kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji. 13 Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.

14 Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na watu wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema, ili kukutana na Israeli katika vita mahali fulani panapotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji. 15 Yoshua na Israeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani. 16 Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji. 17 Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.

18 Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai. 19 Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mavizioni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbilia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.

20 Watu wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wanawakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao. 21 Basi Yoshua na Israeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kutoka kwenye mji, wakawageukia watu wa Ai na kuwashambulia. 22 Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka. 23 Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.

24 Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini. 25 Watu kumi na mbili elfu, waume kwa wake, waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai. 26 Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai. 27 Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile Bwana alivyokuwa amemwagiza Yoshua.

28 Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo. 29 Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo mpaka jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe makubwa mengi juu yake, ambayo yamesalia mpaka leo.

Agano Linafanywa Upya Katika Mlima Ebali
30 Kisha Yoshua akajenga madhabahu ya Bwana, Mungu wa Israeli, katika Mlima wa Ebali, 31 kama Mose mtumishi wa Bwana alivyokuwa amewaamuru Waisraeli. Akaijenga sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Mose: madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo juu yake hakuna chombo cha chuma kilichotumika. Hapo juu yake wakamtolea Bwana sadaka za kuteketezwa na kutoa sadaka za amani.*Sadaka za ushirika. 32 Pale, mbele ya Waisraeli Yoshua akanakili juu ya hayo mawe sheria ya Mose, aliyokuwa ameiandika. 33 Israeli yote, wageni na wazawa sawasawa, wakiwa na wazee wao, maafisa na waamuzi, walikuwa wamesimama pande zote mbili za Sanduku la Agano la Bwana, wakiwaelekea wale waliokuwa wamelichukua, yaani makuhani, ambao ni Walawi. Nusu ya watu ilisimama mbele ya Mlima Gerizimu na nusu hiyo ingine ikasimama mbele ya Mlima Ebali, kama vile Mose mtumishi wa Bwana alivyokuwa ameamuru hapo mwanzo alipotoa maagizo ya kuwabariki watu wa Israeli.

34 Hatimaye, Yoshua akasoma maneno yote ya sheria, yaani baraka na laana, kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria. 35 Hakuna neno lolote katika yale yote ambayo Mose alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakulisomea kusanyiko lote la Israeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na wageni walioishi miongoni mwao.

<- Yoshua 7Yoshua 9 ->
  • Yoshua
  • a