1 Kusanyiko lote la Waisraeli likakusanyika huko Shilo na kusimamisha Hema la Kukutania. Nchi ikawa chini ya utawala wao, 2 lakini palikuwa bado makabila saba ya Israeli ambayo yalikuwa hayajapokea urithi wao.
3 Hivyo Yoshua akawaambia Waisraeli, “Je, mtasubiri hata lini ili kuingia kumiliki nchi ambayo Bwana, Mungu wa baba zenu, amewapa? 4 Chagueni watu watatu kutoka kwenye kila kabila. Nitawatuma hao watu kukagua hiyo nchi na kuniandikia mapendekezo ya mgawanyo wa urithi wa kila kabila. Nao watanirudia. 5 Mtaigawanya hiyo nchi katika sehemu saba. Yuda atabaki katika eneo lake upande wa kusini na nyumba ya Yosefu katika nchi yake upande wa kaskazini. 6 Baada ya kuandika maelezo ya hizo sehemu saba za nchi, yaleteni kwangu, nami nitawapigia kura kwa kura mbele za Bwana Mungu wetu. 7 Hata hivyo, Walawi hawatakuwa na sehemu miongoni mwenu, kwa maana huduma ya ukuhani kwa Bwana ndio urithi wao. Nao Gadi, Reubeni na nusu ya kabila la Manase wameshapata urithi wao upande wa mashariki mwa Yordani, ambako Mose mtumishi wa Bwana aliwapa.”
8 Watu hao walipokuwa wanaondoka kwenda kuandika vizuri kuhusu hiyo nchi, Yoshua akawaagiza, “Nendeni mkakague hiyo nchi na mwandike maelezo kuihusu. Kisha mrudi kwangu, nami nitawapigia kura hapa Shilo mbele za Bwana.” 9 Ndipo hao watu walipoondoka na kupita katika ile nchi. Wakaandika maelezo yake kwenye kitabu, mji kwa mji, katika sehemu saba na kurudisha taarifa kwa Yoshua huko kambini Shilo. 10 Basi Yoshua akawapigia kura huko Shilo mbele za Bwana, na hapo akagawanya ile nchi kwa Waisraeli kufuatana na mgawanyo wa kabila zao.
Mgawo Kwa Benyamini
11 Kura iliangukia kabila la Benyamini, ukoo kwa ukoo. Eneo lao walilogawiwa lilikuwa kati ya kabila la Yuda na la Yosefu.
12 Upande wa kaskazini mpaka wao ulianzia pale Yordani, kupitia kaskazini ya mteremko wa Yeriko na kuendelea magharibi kuingia katika nchi ya vilima, ukitokea kwenye jangwa la Beth-Aveni. 13 Kutoka hapo ulikatiza kwenye mteremko wa kusini mwa Luzu (yaani Betheli) na kushuka hadi Ataroth-Adari katika kilima kusini mwa Beth-Horoni ya Chini.
14 Kutoka kilima kinachotazamana na Beth-Horoni upande wa kusini mpaka ule ukazunguka kusini kufuatia upande wa magharibi, na ukatokezea Kiriath-Baali (yaani Kiriath-Yearimu), mji wa watu wa Yuda. Huu ndio uliokuwa upande wa magharibi.
15 Upande wa kusini mpaka ulianzia kwenye viunga vya Kiriath-Yearimu kwa upande wa magharibi, nao ukatokeza kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa. 16 Mpaka ukateremka hadi shefela inayotazamana na Bonde la Ben-Hinomu, kaskazini mwa Bonde la Refaimu. Ukaendelea chini kwenye Bonde la Hinomu sambamba na mteremko wa kusini mwa mji mkubwa wa Wayebusi na kisha hadi En-Rogeli. 17 Kisha ukapinda kuelekea kaskazini, ukaenda hadi En-Shemeshi na kuendelea mpaka Gelilothi, inayotazamana na Njia ya Adumimu, ukateremka hadi kwenye Jiwe la Bohani mwana wa Reubeni. 18 Ukaendelea upande wa mteremko wa kaskazini wa Beth-Araba ukateremka hadi Araba. 19 Kisha ukaenda mpaka kwenye mteremko wa kaskazini wa Beth-Hogla na kujitokeza kwenye ghuba ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, kwenye maingilio ya Yordani upande wa kusini. Huo ulikuwa mpaka wa kusini.
20 Nayo Yordani ikawa ndio mpaka wa upande wa mashariki.
Hii ilikuwa ndiyo mipaka iliyoonyesha urithi wa koo za Benyamini pande zote.
21 Kabila ya Benyamini, ukoo kwa ukoo, ilikuwa na miji mikubwa ifuatayo:
Yeriko, Beth-Hogla, Emeki-Kesisi, 22 Beth-Araba, Semaraimu, Betheli, 23 Avimu, Para na Ofra, 24 Kefar-Amoni, Ofni, na Geba; miji kumi na miwili pamoja na vijiji vyake.
25 Gibeoni, Rama na Beerothi, 26 Mispa, Kefira, Moza, 27 Rekemu, Irpeeli, Tarala, 28 Zela, Elefu, mji wa Wayebusi (yaani Yerusalemu), Gibea na Kiriathi; miji kumi na minne pamoja na vijiji vyake.