10 “Sasa basi, kama vile Bwana alivyoahidi, ameniweka hai kwa miaka arobaini na mitano tangu wakati alipomwambia Mose jambo hili, wakati Waisraeli wakiwa wanazunguka jangwani. Hivyo mimi hapa leo, nina umri wa miaka themanini na mitano! 11 Bado ninazo nguvu kama siku ile Mose aliponituma. Bado ninazo nguvu za kwenda vitani sasa kama vile nilivyokuwa wakati ule. 12 Basi nipe nchi hii ya vilima, ambayo Bwana aliniahidi siku ile. Wewe mwenyewe ulisikia wakati ule kwamba Waanaki walikuwako huko na miji yao ilikuwa mikubwa na yenye maboma, lakini, kwa msaada wa Bwana, nitawafukuza watoke huko kama vile alivyonena.”
13 Ndipo Yoshua akambariki Kalebu mwana wa Yefune, na akampa Hebroni kama urithi wake. 14 Hivyo Hebroni imekuwa mali ya Kalebu mwana wa Yefune Mkenizi tangu wakati ule, kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wote. 15 (Hebroni uliitwa Kiriath-Arba hapo mwanzo, kutokana na huyo Arba ambaye alikuwa mtu mkuu kupita wote miongoni mwa Waanaki.)