6 Yesu akawaambia, “Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. 7 Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba pia. Tangu sasa, mnamjua Baba yangu, tena mmemwona.”
8 Filipo akamwambia, “Bwana, tuonyeshe Baba yako yatosha.”
9 Yesu akamjibu, “Filipo, nimekaa nanyi muda huu wote hata usinijue? Mtu yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba. Sasa wawezaje kusema, ‘Tuonyeshe Baba’? 10 Je, huamini ya kuwa mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambia siyasemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba akaaye ndani yangu ndiye atendaye hizi kazi. 11 Nisadiki mimi kwamba niko ndani ya Baba na Baba yuko ndani yangu, la sivyo, niaminini kwa sababu ya zile kazi nizitendazo. 12 Amin, amin nawaambia, yeyote aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo yeye atazifanya, naam na kubwa kuliko hizi atazifanya, kwa sababu mimi ninakwenda kwa Baba. 13 Nanyi mkiomba lolote kwa Jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba apate kutukuzwa katika Mwana. 14 Kama mkiniomba lolote kwa Jina langu nitalifanya.
22 Ndipo Yuda, siyo Iskariote, akamwambia, “Bwana, itakuwaje kwamba utajidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?”
23 Yesu akamjibu, “Mtu yeyote akinipenda atalishika neno langu na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya makao yetu kwake. 24 Mtu yeyote asiyenipenda hayashiki maneno yangu na maneno niliyowapa si yangu bali ni ya Baba aliyenituma.
25 “Nimewaambia mambo haya yote wakati bado niko pamoja nanyi. 26 Lakini huyo Msaidizi, yaani, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwenu kwa Jina langu, atawafundisha mambo yote na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27 Amani nawaachia, amani yangu nawapa, amani hii niwapayo si kama ile ulimwengu utoayo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiogope.
28 “Mlinisikia nikisema, ‘Ninakwenda zangu, lakini nitarudi tena.’ Kama kweli mngelinipenda mngelifurahi kwa kuwa naenda kwa Baba, kwani Baba ni mkuu kuniliko mimi. 29 Nimewaambia mambo haya kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini. 30 Sitasema nanyi zaidi, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu anakuja, naye hana kitu kwangu, 31 lakini ulimwengu upate kujua kuwa ninampenda Baba, nami hufanya vile Baba alivyoniamuru.