48 Ndipo mbingu na dunia na vyote vilivyomo ndani yake
vitapiga kelele za shangwe juu ya Babeli,
kwa kuwa kutoka kaskazini
waharabu watamshambulia,”
asema Bwana.
49 “Babeli ni lazima aanguke kwa sababu ya kuwaua Waisraeli,
kama vile waliouawa duniani kote
walivyoanguka kwa sababu ya Babeli.
50 Wewe uliyepona upanga,
ondoka wala usikawie!
Mkumbuke Bwana ukiwa katika nchi ya mbali,
na utafakari juu ya Yerusalemu.”
51 “Tumetahayari, kwa maana tumetukanwa
na aibu imefunika nyuso zetu,
kwa sababu wageni wameingia
mahali patakatifu pa nyumba ya Bwana.”
52 “Lakini siku zinakuja,” asema Bwana,
“nitakapoadhibu sanamu zake,
na katika nchi yake yote
waliojeruhiwa watalia kwa maumivu makali.
53 Hata kama Babeli ikifika angani
na kuziimarisha ngome zake ndefu,
nitatuma waharabu dhidi yake,”
asema Bwana.
54 “Sauti ya kilio inasikika kutoka Babeli,
sauti ya uharibifu mkuu
kutoka nchi ya Wakaldayo.
55Bwana ataiangamiza Babeli,
atanyamazisha makelele ya kishindo chake.
Mawimbi ya adui yatanguruma kama maji makuu,
ngurumo ya sauti zao itavuma.
56 Mharabu atakuja dhidi ya Babeli,
mashujaa wake watakamatwa,
nazo pinde zao zitavunjwa.
Kwa kuwa Bwana ni Mungu wa kisasi,
yeye atalipiza kikamilifu.
57 Nitawafanya maafisa wake na wenye busara walewe,
watawala wao, maafisa, pamoja na wapiganaji wao;
watalala milele na hawataamka,”
asema Mfalme, ambaye jina lake ni Bwana Mwenye Nguvu Zote.
58 Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo:
“Ukuta mnene wa Babeli utasawazishwa,
na malango yaliyoinuka yatateketezwa kwa moto;
mataifa yanajichosha bure,
taabu ya mataifa ni nishati tu ya miali ya moto.”
59 Huu ndio ujumbe Yeremia aliompa afisa Seraya mwana wa Neria mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa utawala wake. 60 Yeremia alikuwa ameandika ndani ya kitabu kuhusu maafa yote yatakayoipata Babeli, yaani yote yaliyokuwa yameandikwa kuhusu Babeli. 61 Yeremia akamwambia Seraya, “Utakapofika Babeli, hakikisha kwamba umesoma maneno haya yote kwa sauti kubwa. 62 Kisha sema, ‘Ee Bwana, umesema utaangamiza mahali hapa ili mtu wala mnyama asiishi ndani yake, napo patakuwa ukiwa milele.’ 63 Utakapomaliza kusoma hiki kitabu, kifungie jiwe kisha ukitupe ndani ya Mto Frati. 64 Kisha sema, ‘Hivi ndivyo Babeli utakavyozama na usiinuke tena, kwa sababu ya maafa nitakayoleta juu yake. Nao watu wake wataanguka.’ ”