7 Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia mwana wa Ahikamu kuwa mtawala wa nchi, na amemweka kuwa kiongozi wa wanaume, wanawake na watoto waliokuwa maskini zaidi katika nchi ambao hawakuchukuliwa kwenda uhamishoni Babeli, 8 wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani na Yonathani wana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi, wana wa Efai Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. 9 Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema: “Msiogope kuwatumikia Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu. 10 Mimi mwenyewe nitakaa Mispa ili kuwawakilisha mbele ya Wakaldayo wanaotujia, lakini ninyi mtavuna divai, matunda ya kiangazi na mafuta, nanyi mtaweka katika vyombo vyenu vya kuhifadhia, na kuishi katika miji mliyojitwalia.”
11 Wayahudi wote waliokuwa Moabu, Amoni, Edomu na nchi nyingine zote waliposikia kwamba mfalme wa Babeli ameacha mabaki ya watu katika Yuda na amemweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani kuwa mtawala wao, 12 wakarudi wote katika nchi ya Yuda kwa Gedalia huko Mispa, kutoka nchi zote ambazo walikuwa wametawanywa. Nao wakavuna divai na matunda tele wakati wa kiangazi.
13 Yohanani mwana wa Karea pamoja na maafisa wote wa jeshi waliokuwa bado wapo kwenye eneo la wazi wakamjia Gedalia huko Mispa 14 na kumwambia, “Je, hujui kwamba Baalisi mfalme wa Waamoni amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania akuue?” Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu hakuwaamini.
15 Kisha Yohanani mwana wa Karea akamwambia Gedalia kwa siri huko Mispa, “Acha niende nikamuue Ishmaeli mwana wa Nethania, wala hakuna atakayejua. Kwa nini akuue na kusababisha Wayahudi wote waliokuzunguka watawanyike, na mabaki wa Yuda waangamie?”
16 Lakini Gedalia mwana wa Ahikamu akamwambia Yohanani mwana wa Karea, “Usifanye jambo kama hilo! Unalosema kuhusu Ishmaeli si kweli.”
<- Yeremia 39Yeremia 41 ->