6 Wakati wa utawala wa Mfalme Yosia, Bwana aliniambia, “Umeona kile Israeli asiye mwaminifu amekifanya? Amepanda juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti uliotanda na amefanya uzinzi huko. 7 Mimi nilifikiri kuwa baada ya kuyafanya yote haya angelinirudia, lakini hakurudi, naye dada yake Yuda mdanganyifu aliona hili. 8 Nilimpa Israeli asiye mwaminifu hati yake ya talaka, na kumfukuza kwa ajili ya uzinzi wake wote. Hata hivyo nikaona kuwa Yuda dada yake mdanganyifu hakuogopa. Yeye pia alitoka na kufanya uzinzi. 9 Kwa sababu uasherati wa Israeli haukuwa kitu kwake, Yuda aliinajisi nchi kwa kuzini na mawe na miti. 10 Pamoja na hayo yote, Yuda dada yake mdanganyifu hakunirudia kwa moyo wake wote, bali kwa kujifanya tu,” asema Bwana.
11Bwana akaniambia, “Israeli asiye mwaminifu ana haki kuliko Yuda mdanganyifu. 12 Nenda, ukatangaze ujumbe huu kuelekea kaskazini:
“ ‘Rudi, Israeli usiye mwaminifu,’ asema Bwana,
‘sitakutazama tena kwa uso uliokunjamana,
kwa kuwa mimi ni mwenye huruma,’ asema Bwana,
‘Sitashika hasira yangu milele.
13 Ungama dhambi zako tu:
kwamba umemwasi Bwana Mungu wako,
umetapanya wema wako kwa miungu ya kigeni
chini ya kila mti unaotanda,
nawe hukunitii mimi,’ ”
asema Bwana.
14 “Rudini, enyi watu msio waaminifu, kwa kuwa mimi ni mume wenu,” asema Bwana. “Nitawachagua ninyi, mmoja kutoka kwenye mji, na wawili kutoka kwenye ukoo, nami nitawaleta Sayuni. 15 Kisha nitawapeni wachungaji wanipendezao moyo wangu, ambao watawaongoza kwa maarifa na ufahamu. 16 Katika siku hizo, idadi yenu itakapokuwa imeongezeka sana katika nchi, watu hawatasema tena, ‘Sanduku la Agano la Bwana,’ ” asema Bwana. “Halitaingia tena kwenye mawazo yao wala kukumbukwa, hawatalihitaji wala halitatengenezwa jingine. 17 Wakati huo, wataita Yerusalemu kuwa Kiti cha Enzi cha Bwana, nayo mataifa yote watakusanyika Yerusalemu kuliheshimu jina la Bwana. Hawatafuata tena ukaidi wa mioyo yao miovu. 18 Katika siku hizo, nyumba ya Yuda itaungana na nyumba ya Israeli, wao kwa pamoja watakuja kutoka nchi ya kaskazini hadi nchi niliyowapa baba zenu kama urithi.
19 “Mimi mwenyewe nilisema,
“ ‘Tazama jinsi nitakavyowatunza kwa furaha kama wana
na kuwapa nchi nzuri,
urithi ulio mzuri kuliko wa taifa jingine lolote.’
Nilidhani mngeniita ‘Baba,’
na msingegeuka, mkaacha kunifuata.
20 Lakini kama mwanamke asiye mwaminifu kwa mumewe,
vivyo hivyo mmekosa uaminifu kwangu pia, ee nyumba ya Israeli,”
asema Bwana.
21 Kilio kinasikika juu ya miinuko iliyo kame,
kulia na kuomboleza kwa watu wa Israeli,
kwa sababu wamepotoka katika njia zao
na wamemsahau Bwana Mungu wao.
22 “Rudini, enyi watu msio waaminifu,
nami nitawaponya ukengeufu wenu.”
“Naam, tutakuja kwako,
kwa maana wewe ni Bwana Mungu wetu.
23 Hakika zile ghasia za kuabudu sanamu kwenye vilima