5 Ndipo nabii Yeremia akamjibu nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama ndani ya nyumba ya Bwana. 6 Akasema, “Amen! Bwana na afanye hivyo! Bwana na ayatimize maneno uliyotoa unabii kwa kuvirudisha mahali hapa kutoka Babeli vyombo vya nyumba ya Bwana pamoja na wote waliohamishwa. 7 Hata hivyo, nisikilize nikuambie yale nitakayoyasema masikioni mwako na masikioni mwa watu hawa wote: 8 Tangu mwanzo, manabii waliokutangulia wewe na mimi walitabiri vita, maafa na tauni dhidi ya nchi nyingi na falme kubwa. 9 Lakini nabii atakayetabiri amani atatambuliwa kuwa kweli ametumwa na Bwana ikiwa unabii wake utatimia.”
10 Kisha nabii Hanania akaiondoa nira iliyokuwa shingoni mwa Yeremia na kuivunja, 11 naye akasema mbele ya watu wote, “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Vivi hivi ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadneza mfalme wa Babeli kutoka kwenye shingo za mataifa katika muda huu wa miaka miwili.’ ” Alipofanya hivi, nabii Yeremia akaondoka zake.
12 Kitambo kidogo baada ya nabii Hanania kuivunja nira kutoka shingo ya nabii Yeremia, neno la Bwana likamjia Yeremia: 13 “Nenda ukamwambie Hanania, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Umevunja nira ya mti, lakini badala yake utapata nira ya chuma. 14 Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Nitaweka nira ya chuma kwenye shingo za mataifa haya yote ili kufanya yamtumikie Nebukadneza mfalme wa Babeli, nao watamtumikia. Nitampa kutawala hata wanyama wa mwituni.’ ”
15 Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, “Sikiliza Hanania! Bwana hajakutuma, lakini wewe umelishawishi taifa hili kuamini uongo. 16 Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana: ‘Hivi karibuni nitakuondoa kutoka juu ya uso wa dunia. Mwaka huu utakufa, kwa sababu umetangaza uasi dhidi ya Bwana.’ ”
17 Katika mwezi wa saba wa mwaka ule ule, nabii Hanania akafa.
<- Yeremia 27Yeremia 29 ->-
Yekonia au Konia ni jina jingine la Yehoyakini.