7 “ ‘Nitaiharibu mipango ya Yuda na Yerusalemu mahali hapa. Nitawafanya waanguke kwa upanga mbele ya adui zao, katika mikono ya wale watafutao uhai wao, nami nitaitoa mizoga yao kuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi. 8 Nitauharibu mji huu na kuufanya kitu cha kudharauliwa. Wote wapitao karibu watashangaa na kuudhihaki kwa sababu ya majeraha yake yote. 9 Nitawafanya wao kula nyama ya wana wao na binti zao; kila mmoja atakula nyama ya mwenzake wakati wa dhiki ya kuzungukwa na jeshi lililowekwa juu yao na adui wanaotafuta uhai wao.’
10 “Kisha livunje lile gudulia wale walio pamoja nawe wakiwa wanaangalia, 11 uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: Nitalivunja taifa hili na mji huu kama gudulia hili la mfinyanzi lilivyovunjwa, nalo haliwezi kutengenezeka tena. Watawazika waliokufa huko Tofethi hata isiwepo nafasi zaidi. 12 Hivi ndivyo nitakavyopafanya mahali hapa na kwa wale waishio ndani yake, asema Bwana. Nitaufanya mji huu kama Tofethi. 13 Nyumba zilizoko Yerusalemu na zile za wafalme wa Yuda zitatiwa unajisi kama mahali hapa, Tofethi: yaani nyumba zote ambazo walifukiza uvumba juu ya mapaa yake kwa jeshi lote la angani, na kumimina dhabihu za vinywaji kwa miungu mingine.’ ”
14 Kisha Yeremia akarudi kutoka Tofethi, mahali ambapo Bwana alikuwa amemtuma kutoa unabii, akasimama katika ua wa Hekalu la Bwana na kuwaambia watu wote, 15 “Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Sikilizeni! Nitaleta juu ya mji huu pamoja na vijiji vinavyouzunguka kila maafa niliyosema dhidi yake, kwa sababu wamekuwa na shingo ngumu, na hawakuyasikiliza maneno yangu.’ ”
<- Yeremia 18Yeremia 20 ->